AU yaitisha mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mabadiliko ya serikali yasiyofuata katiba barani Afrika
2022-03-18 08:36:47| CRI

Umoja wa Afrika (AU) umeitisha mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mabadiliko ya serikali yasiyofuata katiba katika nchi za bara hilo, kwa lengo la kutafuta suluhisho la kukabiliana na matukio yanayojirudia ya kubadili serikali bila kufuata katiba katika bara hilo.

Taarifa iliyotolewa na Umoja huo imesema, Mkutano wa Kutathmini Mabadiliko ya Serikali Yasiyofuata Katiba ulifanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 mwezi huu mjini Accra, Ghana, na kubadilishana maoni kuhusu mapungufu katika sekta ya uongozi barani Afrika.

Akihutubia mkutano huo, rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amesema, mkutano huo unatoa jukwaa la kufanya majadiliano kuhusu kuendelea kwa vitendo vya kubadili serikali bila ya kufuata katiba. Amesisitiza umuhimu wa jukwaa hilo kuwa ni ahadi thabiti ya kuzingatia na kufuata katiba na utawala wa sheria, na kupinga wazi aina zote za mabadiliko ya serikali yasiyofuata katiba katika nchi za Afrika.