Asasi za watu wenye asili ya Khoisan nchini Afrika Kusini zapongeza maamuzi ya mahakama kusitisha ujenzi wa ofisi za Amazon
2022-03-21 14:07:31| CRI

Asasi mbalimbali za wakazi na watu wenye asili ya Khoisan Jumapili zilipongeza maamuzi ya mahakama juu ya ujenzi unaoendelea wa mradi ambao utaweka makao makuu ya kampuni kubwa ya rejareja ya Marekani ya Amazon.

Asasi ya kiraia ya Uchunguzi inayowakilisha Baraza la Kimila la Goringhaicona la watu wenye asili ya Khoisan na Asasi ya Uchunguzi ya wakazi zimesema kwenye taarifa kwamba zimeiomba mahakama kutoa katazo la haraka juu ya mradi huo wakisema utaharibu urithi usioshikika wa eneo takatifu na kwenda kinyume na sera mbalimbali endelevu za kimazingira.

Mradi huo uitwao River Club, unaogharimu rand bilioni 4 sawa na dola milioni 270 za kimarekani, utatoa eneo la ofisi lenye mita za mraba 150,000, na kutarajiwa kuleta faida za uchumi kama vile kutoa ajira za moja kwa moja 5,000 na zisizo za moja kwa moja 13,700 wakati wa hatua ya ujenzi, na kuchochea maendeleo ya biashara.

Ijumaa jaji wa mahakama kuu Patricia Goliath alitoa hukumu ya kusimamisha mara moja ujenzi huo kwani haki za msingi za kiutamaduni na urithi wa watu wa asili, hasa Wakhoi na Wasan zipo hatarini ikiwa hakuna mashauriano sahihi.