Serikali ya Ethiopia na washirika watoa msaada kwa watu milioni 6.4 walioathiriwa na ukame
2022-03-22 09:50:58| CRI

Serikali ya Ethiopia Jumatatu ilisema msaada wa kibinadamu “unaendelea vyema” ukiwalenga watu takriban milioni 6.4 walioathiriwa na ukame katika baadhi ya sehemu nchini Ethiopia.

Shirika la habari la serikali ya Ethiopia (ENA) limeripoti kuwa, hayo yamesemwa na kamishna wa Tume ya Kudhibiti Hatari ya Maafa ya Ethiopia Mitiku Kassa, akieleza kuwa msaada huo unatolewa na serikali ya Ethiopia kwa kushirikiana na washirika mbalimbali wa kibinadamu.

Kassa amesema jamii kwenye sehemu za kusini, kusini-mashariki na nyanda za chini nchini Ethiopia zimeathiriwa na ukame unaoendelea, ambapo msaada wa kuokoa maisha unawasilishwa na muungano wa watendaji wa kibinadamu unaoundwa na serikali, washirika wa kimataifa na nchi za kanda hiyo kwenye sehemu zilizoathiriwa.

Habari nyingine zimesema kuwa, waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Fred Matiangi amesema, kwa mujibu wa makadirio ya mamlaka ya hali ya hewa, waathiriwa wa ukame nchini Kenya wanatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 3.5 ifikapo mwishoni mwa mwezi Mei.