WFP yaonya maafa ya kibinadamu yanayosababishwa na ukame nchini Ethiopia
2022-03-23 10:50:05| CRI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Jumanne lilitoa wito wa kuchukuliwa juhudi za haraka na za pamoja ili kuzuia maafa ya kibinadamu yanayosababishwa na ukame nchini Ethiopia.

WFP imesema “mifugo inakufa, mazao yanaharibika, na wastani wa watu milioni 5.7 wanaamka na njaa kila siku kusini-mashariki mwa Ethiopia wakati Pembe ya Afrika ikikabiliwa na ukame mkali zaidi tangu mwaka 1981.”

Kwa mujibu wa WFP, watu takriban milioni 6.8 wameathiriwa na ukame nchini Ethiopia. Uhaba wa maji na malisho unaharibu maisha ya watu, na kuzilazimisha familia kukimbia makazi yao kwenye sehemu ya kusini na kusini-mashariki nchini humo.

Pia imesisitiza msaada wa haraka na mkubwa zaidi ni muhimu ili kuepusha janga kubwa la kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame nchini Ethiopia na kusaidia sehemu hizo kustahimili athari kubwa za hali ya hewa, na kwamba dola za kimarekani milioni 130 zinahitajika haraka ndani ya miezi minne ijayo, ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 3.5 walioathiriwa zaidi na ukame.