UM: Ukame wa kaskazini mashariki mwa Afrika kuwa mbaya zaidi katika miaka 40 iliyopita
2022-03-24 10:51:00| CRI

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema kuwa ukame wa kaskazini mashariki mwa Afrika unatishia kuwa moja ya majanga mabaya zaidi yanayosababishwa na hali ya hewa katika eneo la Pembe ya Afrika katika miaka 40 iliyopita, huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na njaa kutokana na ukame mbaya katika eneo hilo.

OCHA imesema vyanzo vya maji vilivyokauka katika eneo hilo vinawalazimu watu kutembea umbali mrefu kutafuta maji. Migogoro juu ya raslimali chache huongeza hatari ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto. Ofisi hiyo imesema kuwa kwasababu ya uhaba wa maji, ukosefu wa chakula uko katika rekodi ya juu. Kati ya watu milioni 13.1 na milioni 14.1 katika nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia wanatatizika kupata chakula kila siku.

OCHA na washirika wake wa kibinadamu wanatafuta dola za kimarekani bilioni 4.4 za kutoa msaada wa kuokoa maisha na ulinzi kwa takriban watu milioni 30 katika nchi hizo tatu mwaka huu, lakini ufadhili ni mdogo. Aidha inatoa wito wa dharura kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono kwa mashirika yanayokabiliana na ukame katika eneo zima la Pembe ya Afrika.