Shirika la kibinadamu la UM laeleza wasiwasi kuhusu vurugu huko Ituri, DRC
2022-03-29 09:19:11| CRI

Shirika la kibinadamu la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama inayoendelea kuwa mbaya mkoani Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uratibu wa mambo ya kibinadamu OCHA, imesema matumizi ya mabavu yanayopamba moto mkoani humo yamesababisha mauaji ya raia wapatao 400 na watu zaidi ya elfu 83 kupoteza makazi tangu mwanzo wa mwaka huu.

Katika wiki ya pili ya mwezi wa Machi, raia zaidi ya 80 waliuawa huko Ituri. Wafanyakazi wa kibinadamu wameshuhudia ongezeko la mashambulizi dhidi ya kambi za wakimbizi wa ndani na katika maeneo ambako watu wanatafuta hifadhi. Mwaka jana watu zaidi ya elfu 48 waliathiriwa kutokana na uharibifu wa vituo vya afya na shule mkoani Ituri.