Baraza la Biashara la Afrika Mashariki lasema DRC kujiunga na jumuiya kutahimiza biashara
2022-03-31 09:18:25| CRI

Baraza la Biashara la Afrika Mashariki EABC limetoa taarifa ikisema, kujiunga kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kutahimiza biashara katika kanda hiyo.

Viongozi wa nchi wanachama wa EAC jumanne wiki hii walikubali DRC kujiunga na jumuiya hiyo, na kuifanya nchi hiyo kuwa nchi ya saba mwanachama wa jumuiya hiyo.

Taarifa iliyotolewa na EABC imesema kufuatia DRC kujiunga na jumuiya hiyo, biashara inatarajiwa kuongezeka kwa kasi kwa kuwa nchi hiyo inapakana na nchi wanachama watano Sudan Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.

Baraza hilo limesema hatua hiyo ya kihistoria inaifanya jumuiya ya EAC kuwa mahali penye mvuto mkubwa zaidi kwa uwekezaji barani Afrika, ikitoa uchumi wa soko lenye watu milioni 266 na pato la ndani la dola bilioni 243 za kimarekani.