Kenya yatoa wito Afrika kuzingatia mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya maendeleo
2022-04-01 09:30:37| CRI

Kenya imetoa wito watunga sera wa Afrika kutilia maanani katika athari zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi wakati wakitunga mipango ya maendeleo ya kiuchumi.

Waziri wa kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika wa Kenya Bw. Peter Munya, amesema mabadiliko ya tabianchi ni tishio kuu linalokabili malengo ya maendeleo endelevu ya Afrika SDGs.

Bw. Munya amesema hayo katika hotuba yake iliyotolewa kwa niaba yake na katibu mkuu wa wizara hiyo Lawrence Omuhaka katika mkutano wa 24 wa mwaka wa baraza la sera za ngazi ya juu la Muungano wa utafiti wa uchumi wa Afrika (AERC) uliofanyika huko Nairobi.

Bw. Omuhaka amesema mabadiliko ya tabianchi yameleta athari nyingi, na ili kuhimiza ukuaji wa uchumi wa bara hilo na kuepusha matokeo mabaya yatakayotokana na mabadiliko hayo, watafiti wanatakiwa kueleza msimamo thabiti kwa watunga sera wa Afrika katika kusimamia mabadiliko ya tabianchi.