Mamlaka nchini Sudan zafunga madaraja na kutangaza sikukuu ya kitaifa
2022-04-07 08:36:28| CRI

Mamlaka nchini Sudan jana jumatano zilifunga madaraja mengi yanayounganisha miji mingine na mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, na kutangaza rasmi sikukuu ya kitaifa, wakati maandamano yakipangwa kufanyika siku hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Masuala ya Usalama ya nchi hiyo imesema, madaraja yote yatafungwa siku ya jumatano, isipokuwa madaraja ya Suba na Al-Halfaya ambayo yatakuwa wazi. Pia mamlaka za usalama zilifunga barabara kuu za mjini Khartoum na kupeleka vikosi vya usalama katika makao makuu ya jeshi na ikulu.

Wakati huohuo, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri ilitangaza April 6 kuwa siku ya mapumziko nchini Sudan.

Maandamano hayo yaliyoitishwa na kamati za upinzani kutoka Muungano wa Nguvu za Uhuru na Mabadiliko na Shirikisho la Wanataaluma la Sudan, yamekuja wakati wa kumbukumbu ya mapinduzi ya April 6, mwaka 2019, yaliyosababisha kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al-Bashir.