Waziri wa Afya wa Tanzania asema atiwa hofu na ongezeko la saratani
2022-04-11 09:54:15| cri

Waziri wa Afya wa Tanzania Bi. Ummy Mwalimu amesema idadi iliyorikodiwa ya wagonjwa wa saratani nchini humo inatisha.

Bi. Mwalimu amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la Kituo cha matibabu ya saratani kitakachojengwa kwa pamoja kati ya Serikali na Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam. Ameongeza kuwa mamlaka za afya zinarekodi wagonjwa wapya wa sarantani 42,000 kila mwaka, na asilimia 68 ya wagonjwa wamefariki kutokana na ugonjwa huo. Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho, kitasaidia katika uchunguzi na matibabu ya saratani.

Bi. Mwalimu amesema kituo hicho kitawahudumia wagonjwa 120 wa saratani kila siku na kutoa ahueni kwa Taasisi ya Serikali ya Ocean Road inayozidiwa na wagonjwa.

Ameongeza kusema kuwa aina zinazojulikana zaidi nchini Tanzania ni saratani ya matiti, shingo ya kizazi na tezi dume na kwamba wagonjwa wengi wa saratani waligundulika ugonjwa wao ukiwa katika hatua za mwisho, hivyo kuwataka watu kujenga tabia ya kupima saratani mara kwa mara.