Watu wengi wauawa katika mashambulizi ya silaha katikati ya Nigeria
2022-04-12 09:04:07| cri

Watu wengi waliuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na watu wenye silaha wasiojulikana kwenye vijiji kadhaa katikati ya jimbo la Plateau nchini Nigeria siku ya Jumapili.

Simon Bako Lalong, gavana wa jimbo la Plateau jana kupitia msemaji wake alilaani "mashambulizi haya ya kigaidi" katika baadhi ya jamii katika jimbo hilo ambapo watu wengi waliuawa huku nyumba na mali zikiharibiwa.

Lalong alisema ameviagiza vikosi vya usalama "kuwepo kwenye eneo hilo" baada ya mwitikio wao wa awali kusimamisha mashambulizi. Pia aliwataka kuwafuata washambuliaji waliokuwa wakitoroka na kuhakikisha kwamba "wataadhibiwa kwa uhalifu wao."

Afisa mmoja wa usalama ambaye alikataa kutajwa jina lake aliambia shirika la habari la China Xinhua kuwa takriban watu 80 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, na taarifa za kina zitatolewa baadaye na serikali.

Mashambulizi mfululizo ya makundi yenye silaha yametokea kwenye baadhi ya maeneo ya Nigeria katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha vifo vya raia na utekaji nyara wa watu.