Watu milioni 29 wa Afrika Mashariki wakabiliwa na uhaba wa chakula
2022-04-12 09:01:28| CRI

Watu milioni 29 wa Afrika Mashariki wakabiliwa na uhaba wa chakula_fororder_东非粮食安全

Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki IGAD jana lilitoa ripoti mpya mjini Nairobi, Kenya likisema watu zaidi ya milioni 29 wa Afrika Mashariki wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

Shirika la IGAD limesema Afrika Mashariki inakabiliwa na ukosefu wa mvua kwa msimu wa nne mfululizo, na kuziingiza Ethiopia, Kenya, na Somalia kwenye ukame wa muda mrefu zaidi ambao haujashuhudiwa katika miaka 40 iliyopita.

Katibu mtendaji wa IGAD Bw. Workneh Gebeyehu amesema watu takriban milioni 16 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula kutokana na ukame huo wa muda mrefu. Amesema watu wengine wanakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na athari nyingine kama vile migogoro katika Afrika Mashariki na Ulaya, janga la Corona, na changamoto za kiuchumi. Ametoa wito kwa nchi wanachama, wafadhili, na washirika wa kibinadamu kuchukua hatua mara moja kwenye nchi husika, ili kuzuia hali ya msukosuko wa kibinadamu kuwa mbaya zaidi.