Misaada ya kibinadamu yapewa kipaumbele kuhakikisha maisha ya watu baada ya mapigano kaskazini mwa Ethiopia
2023-01-05 08:21:47| CRI

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema usambazaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano kaskazini mwa Ethiopia unapewa kipaumbele ili kuhakikisha maisha ya watu baada ya mapigano.

Katika ripoti yake ya mwitikio wa kibinadamu nchini Ethiopia, Shirika hilo limesema msaada wa kibinadamu umeanza taratibu kuwafikia watu walioathirika na mapigano kaskazini mwa Ethiopia kufuatia kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya serikali ya Ethiopia na kundi la Harakati za Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).

Hata hivyo Shirika hilo limesema, barabara na usambazaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu, hususan katika mkoa wa Tigray, bado ni kipaumbele ili kuhakikisha watu wanaweza kupata ahueni kutokana na mapigano hayo.