Waziri wa Mambo ya Nje wa China asema China itatoa mchango mkubwa zaidi kwenye sekta ya afya Afrika
2023-01-12 08:58:02| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Qin Gang amesema China itatoa mchango mkubwa zaidi kwenye sekta ya afya ya Afrika na kwa maslahi ya watu wake.

Bw. Qin amesema hayo kwenye sherehe ya kukamilika kwa mradi wa makao makuu ya Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Maradhi cha Afrika (Africa CDC) kwenye kitongoji cha kusini cha Addis Ababa.

Bw. Qin amesema ujenzi wa makao makuu ya Africa CDC ni mradi muhimu wa ushirikiano uliotangazwa na Rais Xi Jinping wa China kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika mwaka 2018 mjini Beijing, na pia ni mradi mwingine mkubwa kwa ushirikiano wa China na Afrika kufuatia Kituo cha Mikutano cha Umoja wa Afrika.

Bw. Qin ameeleza imani yake kuwa kutokana na juhudi za pamoja za China na Afrika, Africa CDC itatoa mchango mkubwa zaidi kwenye sekta ya afya na maslahi ya watu wa Afrika, na kuandika ukurasa mpya kwenye historia ya uhusiano kati ya pande hizo mbili.