Morocco yajiondoa kwenye michuano ya Kombe la CHAN 2022
2023-01-13 14:21:19| cri

Shirikisho la Soka la Kifalme la Morocco (FRMF) limetangaza kuwa Morocco imejiondoa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2022 itakayoanza kutimua vumbi leo Januari 13, 2023.

Uamuzi huo wa Morocco unakuja baada ya Algeria kugomea ombi la Morocco la wajumbe wake kusafiri moja kwa moja kutoka Rabat hadi Constantine wakitumia shirika rasmi la ndege la Royal Air Maroc (RAM) ambalo ni mchukuzi rasmi wa timu ya taifa Morocco. Wiki iliyopita, Waziri wa Michezo wa Algeria Abderrazak Sebgag aliapa kwamba nchi yake itawasilisha majibu yake kwa ombi la Morocco kupitia njia rasmi.

“FAF itajibu CAF kupitia njia rasmi. Algeria ina sheria zake, uhuru wake ambao unazingatiwa juu ya yote,” alisema.

Chombo cha habari cha Algeria TAS, hata hivyo, kilisisitiza kuwa matamshi ya Sebgag “yanaashiria kukataa kwa Algeria” ombi la Morocco. Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulizidi mwaka 2021 baada ya Algeria kuishutumu Morocco kuingilia masuala yake ya ndani. Uongozi wa Algeria pia ulifunga anga yake na kukata uhusiano na Morocco.