Somalia na ATMIS vyapongeza kukombolewa kwa miji mitatu muhimu katika operesheni kubwa ya kijeshi
2023-01-19 13:42:45| cri

Serikali ya Somalia na Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) vimepongeza mafanikio yaliyopatikana na vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika kukomboa miji mitatu ya kimkakati ndani ya siku mbili, na kuahidi kuongeza operesheni dhidi ya kundi la Al-Shabaab nchini humo.

Katika taarifa tofauti, Mjumbe maalum wa Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Mohammed El-Amine Souef na serikali ya Somalia zimepongeza kukombolewa kwa miji ya El-Dhere, Harardhere, na Galad katika mkoa wa Galmudug, katikati ya Somalia siku ya jumatatu na jumanne.

Souef amesema Tume ya Umoja wa Afrika itaendelea kutoa uungaji mkono unaotakiwa ili kuhakikisha Somalia inatokomeza ugaidi na shughuli zinazohusiana na ugaidi.

Serikali ya Somalia imesema, miji hiyo mitatu ya kimkakati ambayo imekombolewa kutokana na uungaji mkono wa wakazi wa huko, ilikuwa ngome ya kundi ya Al-Shabaab kwa muongo mmoja uliopita.