Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere wafikia asilimia 80.2
2023-01-20 18:58:13| cri

Naibu Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Wakili Stephen Byabato, amesema utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 za umeme umefikia asilimia 80.2.

Byabato ameyasema hayo wakati Wizara yake ilipotoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma. Kuhusu kazi ya ujazaji maji katika Bwawa la JNHPP, Waziri Byabato amesema, hadi kufikia Januari 16 mwaka huu, kimo cha maji cha Bwawa kilifikia mita 112.48 kutoka usawa wa bahari kutokea kimo cha mita 74 Desemba 22, 2022. Naibu Waziri ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa JNHPP unaenda sanjari na  utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze mkoani Pwani.