Serikali yapongeza Huawe kwa kutoa mafunzo ya ujuzi wa TEHAMA kwa wenyeji
2023-02-02 23:22:03| cri

Serikali ya Tanzania imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 170 katika Mkongo wa Kitaifa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (NICTBB) unaotekelezwa na HUAWEI Tanzania ili kuongeza kasi ya nchi hiyo katika ushindani wa uchumi wa kidijitali.

Akitoa ufafanuzi mjini Dodoma hivi karibuni, wakati akikabidhi vyeti kwa baadhi ya wahitimu 114 wa Tanzania waliohitimu mafunzo yaliyotolewa na kampuni ya Huawei Tanzania kuhusu namna ya kuendesha na kutengeza mtambo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Dkt Jim Yonazi, alisema uwekezaji huo utasukuma uchumi wa nchi kuwa katika uchumi wa kidijitali shindani.

Akiipongeza kampuni ya Huawei Tanzania kwa moyo wa kuwapatia watanzania ujuzi huo, Dk Yonazi alibainisha kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wahitimu kutunza na kuendesha mitambo ya kusambaza umeme ya NICTBB nchini humo kwa uzalendo badala ya kuajiri wataalam kutoka nje ya nchi na kuongeza kuwa vijana kama wataalam pia watakuwa katika nafasi ya kuishauri serikali juu ya njia bora ya kuiendesha na kuiendeleza.