Watu zaidi ya elfu tatu wafariki kwa tetemeko kubwa la ardhi nchini Uturuki na Syria
2023-02-07 08:29:19| CRI

Mamlaka ya Kudhibiti Maafa na Hali ya Dharura ya Uturuki imesema idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea siku ya Jumatatu imefikia hadi 2,316, huku timu za uokoaji zikikimbizana na wakati ili kuokoa watu walionasa chini ya vifusi katika hali ya hewa ya baridi na ya mvua.

Mamlaka hiyo pia imebainisha kuwa watu wasiopungua 14,483 walijeruhiwa na majengo 5,606 kuharibiwa, na kuongeza kuwa jumla ya watu 14,720 kwa sasa wanatoa msaada katika eneo la maafa, ikiwa ni pamoja na wanajeshi.

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha Richter liliukumba mkoa wa kusini wa Uturuki wa Kahramanmaras saa 10 na dakika 17 alfajiri kwa saa za huko, likifuatiwa na matetemeko mengine makubwa ya ardhi. Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kwa wahanga.

Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Syria imesema takriban watu 711 wamefariki na wengine 1,431 kujeruhiwa nchini humo baada ya matetemeko hayo makubwa ya ardhi kutikisa sehemu za kusini mwa Uturuki na jirani yake Syria. Hata hivyo, idadi hiyo haijumuishi sehemu zinazoshikiliwa na waasi katika mkoa wa Idlib na sehemu za vitongoji vya mkoa wa Aleppo.

Serikali ya Syria imeanzisha kituo kikuu cha operesheni cha saa 24 kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa Syria Hussein Arnous ili kuratibu shughuli za misaada ya tetemeko la ardhi, huku wizara, taasisi na mamlaka zote husika zikiwa katika tahadhari.