Idadi ya vifo yafikia 38 kwenye ajali ya treni nchini Ugiriki
2023-03-02 09:02:38| CRI

Idara ya zimamoto ya Ugiriki imesema idadi ya vifo kwenye ajali ya treni mbili zilizogongana uso kwa uso iliyotokea Jumanne usiku katikati mwa nchi hiyo, imeongezeka na kufikia 38 huku watu 57 bado wakiwa wamelazwa hospitali, sita kati yao wakilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

Akizungumza na wanahabari msemaji wa idara hiyo Bw. Vasilios Vathrakogiannis alisema kazi ya uokoaji bado inaendelea kufanyika karibu na mji wa Larissa, na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Rais Xi Jinping wa China ametuma salamu za rambirambi kwa mwenzake wa Ugiriki Katerina Sakellaropoulou kufuatia ajali hiyo. Xi ameeleza kushtushwa kwake na habari ya ajali hiyo iliyosababisha vifo na majeruhi wengi. Kwa niaba ya serikali ya China na watu wake, Xi alitoa salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa, na kuwatakia majeruhi wapone haraka.