Kampuni ya simu ya Kenya inashirikiana na kampuni ya Huawei ya China kuzindua vituo vya 5G
2023-03-17 09:04:02| CRI

Kampuni ya simu za mkononi ya Kenya Safaricom imesema inashirikiana na kampuni ya Huawei ya China, kuzindua vituo vitatu vya huduma ya 5G mjini Nairobi.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Safaricom Bw. Peter Ndegwa amesema vituo hivyo vitatu vitaonyesha kasi ya juu na vifaa vya karibuni vinavyotumia teknoloijia ya 5G. Amesema vituo hivyo vitawawezesha wakenya kutambua nguvu ya huduma ya 5G moja kwa moja.

Kampuni ya Safaricom ilizindua huduma ya 5G mwezi Oktoba mwaka jana, ikiwa ni kampuni ya kwanza kufanya hivyo katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwa na vituo zaidi ya 200 vya huduma ya 5G katika kaunti 11 nchini Kenya.

Amesema kwa sasa zaidi ya wateja laki 3 wa Safaricom tayari wanatumia simu zinaztumia huduma ya 5G, na wanaweza kupata kasi ya 2Gbps, na kasi ya kawaida ya 400Mbps hadi 700Mbps.