Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe asema uwekezaji wa China umechangia ukuaji wa uchumi wa Zimababwe
2023-06-01 14:36:04| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Dkt. Frederick Shava ambaye alikuwa ziarani mjini Beijing, amesema kuwa China ni mwenzi muhimu wa biashara, na pia ni chanzo kikuu cha uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia kwa Zimbabwe, na kusisitiza kwamba Zimbabwe itaendelea kuimarisha ushirikiano na China na kuendelea kupanua uwekezaji na biashara kati ya pande hizo mbili.

Dkt. Shava amesema hayo alipohutubia ufunguzi wa Baraza la Biashara kati ya China na Zimbabwe lililofunguliwa Mei 30 hapa Beijing. Waziri huyo amesema, kutokana na juhudi za pamoja za Zimbabwe na China, katika miaka ya hivi karibuni biashara kati ya nchi hizo mbili imeendelea kukua. Mwaka 2022, Zimbabwe iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.125, zikiwemo vifaa na mashine za viwandani, dawa, dawa za kilimo na magari kutoka China, na mwaka huo huo, nchi hiyo iliuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.3 kwa China, zikiwemo tumbaku, matunda, ngozi za wanyama, chuma na madini.

Dkt. Shava amesema, China imekuwa nchi ya tatu inayonunua kwa wingi zaidi bidhaa za Zimbabwe, na nchi hizo mbili bado zina mustakabali mkubwa wa kupanua zaidi biashara kati yao. Amesema kutokana na mkataba uliosainiwa mwaka 2021, matunda jamii ya machungwa yanayozalishwa nchini Zimbabwe yameweza kuingia kwenye soko la China. Hivi sasa hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kuhimiza usafirishaji wa bidhaa nyingine za kilimo kama vile parachichi, karanga, pecan, ufuta,pilipili, nyama ya mbuzi na ng’ombe kutoka Zimbabwe hadi soko la China. Dkt. Shava anatarajia kuwa nchi yake itaweza kupanua zaidi aina za bidhaa zinazosafirishwa China, na kuongeza zaidi uuzaji wa bidhaa zilizochakatwa kwenye soko la China.

Akizungumzia uwekezaji wa pande mbili, Dkt. Shava amesema China ni chanzo kikubwa zaidi cha uwekezaji wa moja kwa moja kwa Zimbabwe, na uwekezaji wa China umekwenda zaidi kwenye sekta za madini, utengenezaji bidhaa, kilimo, ujenzi, uchukuzi na utalii. Katika miaka minne iliyopita, China imewekeza dola za kimarekani bilioni 2.7 nchini Zimbabwe, na Zimbabwe imetoa vibali zaidi ya 400 vya uwekezaji kwa kampuni za China. Dkt. Shava amesema, uwekezaji kutoka China umetoa nafasi za ajira, kuhimiza maendeleo ya miundombinu, kuendeleza sekta za madini, utengenezaji bidhaa na kilimo ziwe za kisasa, na hivyo kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa Zimbabwe.

Waziri Shava amezialika kampuni za China kuwekeza zaidi nchini Zimbabwe, na kuimarisha ushirikiano kwenye nyanja za biashara ya mashine na vifaa, uchakataji wa bidhaa za kilimo, ujenzi wa hoteli na viwanja vya gofu na ujenzi wa miundombinu. Amesema, kupitia kuhimiza biashara na uwekezaji kati ya pande hizo mbili, uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya Zimbabwe na China hakika utaendelea kupiga hatua hadi kwenye ngazi mpya.