Tanzania yatoa wito wa kufanyika juhudi zaidi za kulinda Bahari ya Hindi isichafuliwe na plastiki
2024-06-06 08:55:03| CRI

Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango ametoa wito wa kufanyika juhudi za pamoja ili kulinda Bahari ya Hindi na fukwe zake zisichafuliwe na plastiki.

Akihutubia taifa mjini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani jana Jumatano, Mpango alisema Bahari ya Hindi ya Tanzania na fukwe zake zimechafuliwa na plastiki, jambo ambalo linaweka hatarini rasilimali za baharini. Alieleza kuwa wataalamu kote duniani wametabiri kwamba kufikia mwaka 2050, kutakuwa na plastiki nyingi zaidi katika bahari kuliko rasilimali za uvuvi, akitoa wito wa juhudi zaidi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza sera zaidi na kuongeza uelewa wa watu ili kulinda bahari.

Aliongeza kuwa plastiki zinazotupwa baharini hutoa sumu ambazo ni hatari kwa rasilimali za baharini na binadamu.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa tarehe 5 Juni kila mwaka, ikihamasisha uelewa na hatua za kulinda mazingira. Mwaka huu, kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani ni "Urejeshaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame."