Kenya Jumatano ilianzisha sekretarieti ya kampeni ili kufanya kazi na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika azma yake ya kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Akihutubia mkutano wa pamoja na Odinga mjini Nairobi, Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Diaspora Musalia Mudavadi, amesema Kampeni hiyo itaongozwa na maafisa wenye uzoefu na ujuzi wa hali ya juu. Sekretarieti itakuwa na jukumu la kuandaa muhtasari wote muhimu kwa mgombea, kuandaa vifaa vya kampeni, na kuandaa mjadala wa hadhara utakaotangazwa moja kwa moja barani Afrika.
Kwa upande wake Odinga alisema kama atapata uenyekiti wa AUC, anaazimia kubadilisha sura ya Afrika na kulifanya kuwa bara lenye nguvu kiuchumi. Awali Odinga alihudumu kama Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika kwa Maendeleo ya Miundombinu hadi muda wake ulipokamilika mwaka 2023.