Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema, mvua kubwa, mafuriko na mapigano makali yanayoendelea yamesababisha hali kuwa mbaya zaidi nchini Sudan.
Ofisi hiyo imesema, mvua kubwa na mafuriko vimeathiri watu 143,000 katika mikoa 12 kati ya 18 ya nchini Sudan. Pia OCHA imesema mafuriko yamesababisha watu 27,000 kukosa makazi tangu mwezi Juni, huku mji wa El Fasher ukiwa umeathirika zaidi.
Wakati huohuo, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limeripoti kuwa limegawa chakula kwa karibu watu 14,000 katika eneo la Sheikan, mkoa wa Kordofan Kaskazini, ambalo ni moja ya maeneo yaliyofanyiwa tathmini na Kamati ya Kutathmini Njaa (IPC), kuwa liko katika hatari ya kukabiliwa na ukosefu wa chakula.