Watu 800,000 wakimbilia Sudan Kusini kuepuka mapigano nchini Sudan
2024-08-15 08:59:41| CRI

Waziri wa Masuala ya Kibinadamu na Usimamizi wa Majanga wa nchini Sudan Kusini, Albino Akol Atak amesema, mapigano yanayoendelea nchini Sudan kati ya Jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha RSF yamewalazimisha watu zaidi ya 800,000 kukimbilia nchini Sudan Kusini tangu mwezi April mwaka jana.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada wa chakula uliotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba, Bw. Atak amesema mwaka huu Sudan Kusini imekabiliwa na migogoro mingi ambayo imehatarisha maisha ya wananchi wake, moja ikiwa ni athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha mafuriko na ukame, na nyingine ni mapigano ya nchini Sudan yaliyolazimisha zaidi ya watu 800,000 kukimbilia nchini Sudan Kusini.

Mkurugenzi wa WFP na mwakilishi wa Shirika hilo nchini Sudan Kusini Mary-Ellen McGroaty amesema, WFP inakabiliwa na upungudu wa dola za kimarekani milioni 270 ili kukabiliana na athari za mafuriko, mgogoro unaoendelea nchini Sudan, uhaba wa chakula na mgogoro wa utapiamlo nchini Sudan Kusini.