Rais Xi Jinping wa China jana Jumanne alikutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Fiji Bw. Sitiveni Rabuka hapa Beijing.
Rais Xi amepongeza timu ya raga ya wanaume ya Fiji kupata medali ya fedha kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris.
Akiitaja Fiji kuwa nchi ya kwanza ya kisiwa ya Pasifiki kuanzisha uhusiano wa kibalozi na China na kwamba mwaka kesho utakuwa maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa nchi hizo mbili, Rais Xi amesema, katika nusu karne iliyopita, China na Fiji zimekuwa zikiungana mikono na kusaidiana, na kuweka mfano wa kuigwa wa kutendeana kwa usawa na ushirikiano wa kirafiki kati ya nchi kubwa na nchi ndogo.
Rais Xi amesema, China inatilia maanani uhusiano na Fiji na inapenda kutoa msaada kadri inavyoweza kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Fiji, na kushirikiana na Fiji katika kuelekeza mwelekeo wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuhimiza ujenzi wa Jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Fiji ili kunufaisha zaidi watu wa nchi hizo mbili.