China yasaidia nchi za Afrika kupunguza shinikizo la madeni
2024-08-21 09:43:44| CRI

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Asia Magharibi na Afrika ya Wizara ya Biashara ya China Shen Xiang, amesema kwenye mkutano na waandishi habari kuwa China imezisaidia nchi nyingi za Afrika kupunguza shinikizo la madeni kupitia njia mbalimbali.

Ameeleza kuwa China imetoa mchango chanya katika shughuli hizo chini ya mfumo wa Pendekezo la G20 la kuahirisha na kupunguza malipo ya deni kwa nchi zinazoendelea. Kupitia mfumo wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, China imesamehe madeni ya nchi za Afrika kwa njia ya mikopo ya serikali isiyo na riba ambayo ilipaswa kuanza kulipwa mwishoni mwa 2021. Mashirika na kampuni za kifedha za China pia zimeshiriki kwenye shughuli za uwekezaji na ushirikiano wa ufadhili wa fedha na nchi za Afrika kwa kufuata kanuni za soko na sheria za kimataifa.

Ameongeza kuwa China siku zote inaheshimu na kuzingatia nia na mahitaji halisi ya nchi za Afrika, na kamwe haiambatanishi na masharti yoyote ya kisiasa, hatua ambazo zimepongezwa na nchi za Afrika.