Jopo la washauri bingwa Zimbabwe: ushirikiano kati ya China na SADC utaimarishwa zaidi
2024-08-29 09:20:34| CRI

Kuchaguliwa kwa Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kutasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya China na Jumuiya hiyo.

Hayo yamesemwa na Munetsi Madakufamba ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Utafiti na Nyaraka Kusini mwa Afrika (SARDC), kituo washirika wa maarifa cha SADC kilichopo mjini Harare, Zimbabwe. Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Bw. Madakufamba alieleza matarajio makubwa ya jopo hilo la washauri bingwa na mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utakaofanyika wiki ijayo mjini Beijing akisema utainua zaidi ushirikiano kati ya China na Zimbabwe na China na SADC.

Madakufamba aliyasema hayo Jumanne kwenye semina ya nusu siku iliyofanyika mjini Harare ambayo ilijadili njia za kuimarisha uhusiano kati ya China na SADC kabla ya Mkutano wa wakuu wa FOCAC. Semina hiyo ilifanyika chini ya ufadhili wa Taasisi ya SARDC ya Mafunzo ya China na Afrika Kusini mwa Afrika ikishirikiana na Kituo cha Mafunzo ya Afrika cha Chuo Kikuu cha Peking.Mnangagwa alichukua uenyekiti wa zamu wa kanda ya SADC katika mkutano wa kilele uliofanyika Zimbabwe mwezi huu.