Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Bwana Othman Masoud Othman, amesisitiza kuwa mabadiliko ni sehemu isiyoepukika ya changamoto za kimataifa na kwamba wakati umefika kwa Zanzibar kukumbatia mabadiliko hayo.
Akiongea na vijana visiwani Zanzibar Bwana Othman amesema vijana ndio vinara wa mabadiliko. Amesisitiza kuwa uungaji mkono wa vijana kwenye harakati zozote za maendeleo unaashiria tumaini kubwa na kuendana na mahitaji yao.
Bwana Othman pia amesisitiza umuhimu wa vijana kuchagua viongozi wanaowataka, na kutumia sehemu hii muhimu ya kijamii kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Lakini pia amekosoa kutokuwepo kwa maono ya muda mrefu miongoni mwa baadhi ya viongozi kuhusu mambo ya vijana, akisema hali hii inasababisha mkanganyiko na kukata tamaa kwa baadhi ya vijana.