Wajumbe wanaohudhuria Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika (AFS) linalofanyika mjini Kigali, Rwanda, wametoa wito wa uvumbuzi wa haraka, uwekezaji na nia ya kisiasa ili kufanya mageuzi ya kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula katika bara hilo.
Jukwaa hilo limekutanisha washiriki zaidi ya 5,000 wakiwemo watunga sera, wawekezaji katika kilimo cha kibiashara, wasomi, mashirika ya wakulima, wawakilishi wa sekta binafsi na vijana, na linalenga kuongeza kasi ya mageuzi ya mifumo ya chakula barani Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Rwanda Edouard Ngirente amesisitiza haja ya uratibu kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wengine ili kutimiza mifumo endelevu ya chakula. Amezitaka serikali za nchi za Afrika kuboresha teknolojia za kidijitali, na kujenga mifumo jumuishi inayohakikisha upatikanaji wa chakula bora na lishe kwa Waafrika wote.