Rais wa China akutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika
2024-09-04 09:53:12| cri

Rais wa China Xi Jinping jana alikutana mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Faki Mahamat kwenye Jumba Kuu la Mikutano ya Umma mjini Beijing.

Rais Xi amesema, katika miaka ya hivi karibuni, China na Umoja wa Afrika zimeendelea kuimarisha kuaminiana kisiasa, kuongeza uratibu na kushirikiana kwa karibu katika masuala ya kimataifa na kikanda. Amesema China inaunga mkono Umoja wa Afrika katika kuchukua nafasi kubwa zaidi katika urafiki kati ya China na Afrika, na inapenda kuchukulia mkutano huo wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kama fursa ya kukuza ushirikiano kati ya China na Umoja wa Afrika katika nyanja mbalimbali ili kupata mafanikio zaidi na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja hadi kufikia ngazi mpya.

Kwa upande wake, Bw. Faki ambaye yuko nchini China kuhudhuria Mkutano wa FOCAC, ameishukuru China kwa kukuza ushirikiano kati ya Afrika na China na kuanzishwa kwa utaratibu wa FOCAC. Amesema Afrika inafuata kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja duniani na inaiunga mkono kwa dhati China katika kutetea maslahi yake makuu.