Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema mahitaji ya zaidi ya wahanga 400,000 wa mafuriko ya kaskazini-mashariki mwa Nigeria ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na msaada wa chakula, maji ya kunywa, usafi wa mazingira na makazi.
OCHA imeeleza kuwa ujumbe wa pamoja wa wakuu wa mashirika ya UM na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na Chama cha Msalaba Mwekundu cha Nigeria ulitembelea Maiduguri mwishoni mwa wiki iliyopita na kukutana na watu walioathirika na maafisa wa serikali. Watu wengi waliokutana nao walihitaji msaada kabla ya mafuriko, wakilazimika kuhama makazi yao mara nyingi kutokana na migogoro na ukosefu wa usalama.
Ofisi hiyo ilisema kuwa kuna umuhimu wa haraka wa shughuli za ulinzi ili kupunguza hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na kuwalinda watoto wasio na wazazi. OCHA ilisema serikali za mitaa ziliripoti kuwa watu 300,000 waliokimbia makazi kwa muda wamesajiliwa tangu Septemba 9 lilipopasuka Bwawa la Alau. Ufikiaji umeendelea kuwa na vikwazo kwani madaraja mawili muhimu huko Maiduguri, miongoni mwa miundombinu mingine muhimu, yameporomoka kiasi.