Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC wa 2024 ulimalizika hivi karibuni mjini Beijing, na kupitisha "Azimio la Beijing" na "Mpango wa Utekelezaji (2025-2027)". Wakati jumuiya ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa, ikipongeza kujumuika tena kwa familia za China na Afrika, ambako kunaashiria kuongezeka kwa nguvu ya "Dunia ya Kusini," watu pia waliona kuwa duru za kimkakati na vyombo vya habari vya Marekani viliuliza kwa nia mbaya: nani ananufaika zaidi? Ni China au Afrika?
Swali hili lililoulizwa kwa makusudi limepuuza kuwa hali ya kunufaishana ni msingi wa ushirikiano kati ya China na Afrika, na nyuma ya swali hilo kuna tabia inayojirudia ya "kuharibu na kuokoa kwa wakati mmoja": kwa upande mmoja, Marekani inajaribu kuchochea vibaya uhusiano kati ya China na Afrika, na kwa upande mwingine, inajitahidi kuokoa hasara ilizopata kutokana na kiburi na ujinga wake kuhusu Afrika katika miongo michache iliyopita. Kwa ufupi, Marekani bado imejaa mtazamo wa umwamba, na inataka kuikandamiza China, kuharibu umoja wa nchi zinazoendelea, na kufikia lengo lake la "kuendelea kuongoza dunia."
Mwaka 2000, jarida maarufu la kimagharibi "The Economist" lilichapisha makala kwenye ukurasa wake wa mbele yenye kichwa cha "bara lisilo na matumaini." Lakini pia mwaka huo huo Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC lilianzishwa, na kuanzia hapo bara la Afrika likawa na sura mpya. China tangu zamani imegundua tatizo kubwa linalozuia maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, yaani miundombinu duni. Katika miaka 24 iliyopita, FOCAC imekuwa na nafasi muhimu katika kukuza maendeleo ya Afrika na kuboresha maisha ya watu wa Afrika, kuisaidia Afrika kujenga na kukarabati reli zenye urefu wa zaidi ya kilomita elfu 10, barabara za karibu kilomita laki 1, madaraja karibu elfu moja na bandari karibu mia moja. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, makampuni ya China yalitoa nafasi za ajira zaidi ya milioni 1.1 barani Afrika.
Sasa kwa kuwa msingi huo umewekwa, Mkutano huo wa Kilele wa FOCAC umefungua kipindi kipya cha ushirikiano kati ya China na Afrika yaani kukuza mambo ya kisasa kwa pamoja. Katika Mkutano huo wa Beijing, China ilitangaza hatua zake muhimu za kuunga mkono Afrika katika miaka mitatu ijayo, ikiwa ni pamoja na biashara, miundombinu, utamaduni, afya na mambo mengine ambayo yanahitaji kuimarishwa kwa haraka kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, kuweka msingi wa ushirikiano kati ya Kusini na Kusini na ushirikiano wa kimataifa na Afrika. Hali halisi ni kuwa, sio tu katika FOCAC, bali pia katika mifumo na dhana zikiwemo BRICS, ujenzi wa pamoja wa hali ya juu wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na Mapendekezo Matatu Duniani, China siku zote imesisitiza kujengwa kwa dunia iliyo na usawa na haki, ambapo "nchi za kusini" zina uwakilishi na sauti zinazostahiki katika masuala ya kimataifa. Mkutano huo wa Beijing umeamua kuinua hali ya jumla ya uhusiano kati ya China na Afrika kuwa jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja wa hali zote katika zama mpya, ambayo ni onyesho kamili la sera hii ya diplomasia ya China. Ni wazi kuwa mafanikio ya mkutano huo wa Beijing si tu ni ya China na Afrika, bali pia ni ushindi wa pamoja kwa dunia ya kusini.
Hata hivyo, kama alivyosema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika Mkutano wa Beijing, "Ushirikiano wa Kusini Kusini ni muhimu katika kujenga uwezo na kuhimiza kufikiwa kwa malengo ya pamoja ya maendeleo, lakini wakati huo huo dunia ya kaskazini haipaswi kusahau majukumu yao." Kwa sababu wakati nchi hizi zilizoendelea zilipotafuta usasa, nchi zinazoendelea zimeteseka sana. Katika kukuza maendeleo ya "dunia ya kusini" ikiwa ni pamoja na Afrika, Marekani haipaswi na haihitaji kupambana na China na hata kuzidisha makabiliano, na badala yake inapaswa kugeuza ahadi moja moja kuwa kitendo halisi kama ilivyofanya China. Kuongezeka kwa nguvu ya "dunia ya kusini" kumekuwa mwelekeo usiozuiliwa, jambo ambalo linaweza kuchukuliwa na Marekani kama tishio, lakini kwa wanachama wengine wengi wa jumuiya ya kimataifa, ni jambo jema—linalotoa fursa ya kuunda utaratibu mpya wa kiuchumi wa kimataifa na kujenga dunia iliyo na haki, ustawi na amani zaidi kwa watu wote.