Sudan yazindua kampeni ya kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu
2024-09-23 08:36:15| CRI

Waziri wa Afya wa Sudan Haitham Mohamed Ibrahim ametangaza uzinduzi wa kampeni ya mwezi mmoja ya kukabiliana na janga la kipindupindu.

Waziri huyo amesema katika taarifa yake kuwa, uamuzi wa kuzindua kampeni hiyo umefikiwa katika mkutano wa dharura wa kamati ya ngazi ya juu zaidi ya masuala ya afya na dharura za kibinadamu huko Kassala, mji mkuu wa Jimbo la Kassala, mashariki mwa Sudan.

Amesema kampeni hiyo inalenga kupambana na ugonjwa wa kipindupindu, kuongeza mwitikio wa ugonjwa huo katika majimbo, kuunganisha juhudi, kutumia uwezo uliopo na kuimarisha umuhimu wa jamii ili kuzingatia usafi wa mazingira.

Mpango wa kampeni hiyo ni pamoja na utoaji wa chanjo, hatua za kushughulia afya ya mazingira, udhibiti wa chakula, na kusafisha maji, na pia kuongeza uelewa wa watu juu ya hatari ya kipindupindu, na hatua za kulinda afya.