Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Lebanon zimeonyesha kuwa mashambulizi ya anga ya Israel yaliyofanywa jana dhidi ya Lebanon yamesababisha vifo vya watu 72 na majeruhi 392.
Vikosi vya Ulinzi vya Israel vimeeleza kuwa shabaha za mashambulizi ya anga ya Israel ni vituo vya kijeshi vya Hezbollah, yakiwemo majengo ya makazi yenye silaha na vifaa, na kusisitiza kuwa jeshi la Israel limetoa tahadhari mapema kwa raia katika maeneo husika kabla ya mashambulizi hayo ya anga.
Israel imeendelea kufanya mashambulizi katika maeneo mengi nchini Lebanon. Waziri wa Mazingira wa serikali ya muda ya Lebanon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Dharura ya Serikali Nasser Yassin amesema kwamba tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Lebanon tarehe 23, watu 1,247 wameuawa na wengine 5,278 wamejeruhiwa, na watu zaidi ya laki moja walioko kusini mwa Lebanon wamekimbia makazi yao, na serikali imepanga maeneo zaidi ya 300 ya makazi mapya.