Messi awahi kukiri nyota wa Barcelona waichukia klabu ya Chelsea zaidi ya Real Madrid
2024-10-02 10:18:33| cri

Lionel Messi aliwahi kukiri kwamba yeye na wachezaji wenzake wa Barcelona walikuwa na uadui mkubwa dhidi ya Chelsea kuliko hata wapinzani wao wakali, Real Madrid.

Ingawa hivi sasa Chelsea inaonekana haina nguvu kubwa Ulaya, lakini katikati hadi mwishoni mwa miaka ya 2000, walikuwa na nguvu kubwa katika hatua za mwisho za Ligi ya Mabingwa. Barcelona mara nyingi walijikuta wakikabiliana na Chelsea, wakipambana mara nane ndani ya miaka mitano pekee. Makabiliano haya mara nyingi yalikuwa ya moto na kujaa mabishano, na kufanya yasisahaulike.

Kabla ya mchuano mkali wa hatua ya 16 bora mwaka 2006, Messi mwenye umri wa miaka 18 alifunguka kuhusu jinsi Barcelona walivyowachukia sana wapinzani wao wa London Magharibi. "Kuna wachezaji hapa ambao wanaichukia Chelsea kuliko Real Madrid," Messi alikiri kwenye Habari za Ulimwengu kupitia Sportskeeda.

"Sikuwahi kufikiria kama nitasema hivyo. Pia sikuwahi kufikiria kama nitashuhudia mchuano mkali zaidi ya Boca dhidi ya River Plate au Brazil dhidi ya Argentina. Afadhali tukabiliane na Arsenal, Manchester United, au timu nyingine yoyote kuliko kuwa uwanja mmoja na Chelsea."