Makampuni ya China yanayofanya kazi nchini Zambia yanapanga kuongeza uwekezaji wao katika sekta ya madini kwa dola bilioni 5 za Marekani katika kipindi cha miaka mitano ijayo na kuongeza uzalishaji hadi tani 280,000 za shaba nchini humo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini wa China nchini Zambia, Li Zhanyan, alisema Jumatatu katika ufunguzi wa Mkutano wa Uchimbaji madini na Uwekezaji nchini Zambia mwaka 2024 kwamba makampuni yamewekeza zaidi ya dola bilioni 3.5 katika sekta ya madini ya Zambia katika miaka 26 iliyopita, yakitoa nafasi za ajira 15,000 na kuzalisha tani 130,000 za shaba safi, tani 250,000 za shaba isiyosafishwa, na tani 50,000 za shaba iliyochujwa kila mwaka.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu ya "Uchimbaji Zaidi ya Shaba; Kuadhimisha Miaka 100 ya Uchimbaji Madini nchini Zambia," unafanyika kuanzia Oktoba 7 hadi 11 mjini Lusaka, Zambia. Ukiwaleta pamoja zaidi ya washiriki 2,500, mkutano huo unatoa jukwaa la kubadilishana maarifa, ushirikiano na uwekezaji ili kuendesha sekta ya madini ya Zambia.