Maonyesho ya 7 ya CIIE yatoa jukwaa la kuonyesha bidhaa na huduma za Tanzania
2024-10-16 08:42:09| CRI

Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yatatoa jukwaa la kuonyesha bidhaa na huduma za Tanzania katika moja ya soko kubwa zaidi duniani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Tanzania Zanzibar, Omar Said Shaaban, katika hafla ya kuwaaga wafanyabiashara wa Tanzania wanaoshiriki maonyesho hayo yaliyofanyika katika Ubalozi wa China nchini Tanzania jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo amesema wafanyabiashara 34 wa Tanzania watashiriki katika Maonyesho ya mwaka huu yatakayofanyika Shanghai kuanzia Novemba 5 hadi 10 mwaka huu, na wataonyesha bidhaa mbalimbali zikiwemo za kilimo, vitambaa, madini, sanaa za mikono na bidhaa za viwandani. Amesema lengo la kushiriki Maonyesho hayo ni kutangaza chapa ya “Made in Tanzania,” ambayo inaleta taswira ya usawa, uendelevu na upekee wa bidhaa za Tanzania.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema, thamani ya biashara kati ya China na Tanzania imefikia dola za kimarekani bilioni 8.78 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la kihistoria la asilimia 8.9 ikilinganishwa na mwaka 2022.