Naibu mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Geng Shuang amesema, China inaitaka jumuiya ya kimataifa kuzingatia madhara ya ukoloni, kuyaondoa na kulinda usawa na haki za kimataifa, na kuhimiza kuanzisha utaratibu wa kimataifa wa haki zaidi.
Akizungumza katika mjadala wa Kamati ya 4 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kuondoa madhara ya ukoloni uliofanyika jana, Balozi Geng amesema China inakaribisha Azimio la kuondoa madhara ya aina zote za ukoloni lililopitishwa na Kamati Maalum ya Kuondoa Ukoloni, na inatarajia azimio hilo litapitishwa katika Kamati ya 4 ya Baraza Kuu.
Pia amesema China inazitaka nchi ambazo zinaendeleza mfumo wa kikoloni au kunufaika nao kuonyesha utashi wa kisiasa, kubeba majukumu ya kihistoria, kufidia matokeo ya ukoloni, kuacha kufuata fikra za kikoloni, kuacha umwamba, kuacha kudhuru maslahi ya nchi nyingine, na kuacha kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine.