Kongamano la China na Afrika kuhusu Kilimo cha Mpunga barani Afrika limefunguliwa jumatano wiki hii katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, kwa kutoa wito wa kupanua kilimo cha mpunga ulioboreshwa katika bara hilo.
Kongamano hilo pia lilijadili jinsi mpunga huo unavyoweza kuboresha usalama wa chakula barani Afrika kwa kutumia mbinu za kiuvumbuzi za kilimo na kutumia vizuri uhusiano wa kimkakati kati ya China na Afrika katika sekta ya kilimo.
Akizungumza katika kongamano hilo, Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Bluu na Mazingira Endelevu, Josefa Leonel Sacko amesema, Afrika haijitoshelezi kwa uzalishaji wa mpunga na inategemea kwa kiasi kikubwa uagizaji kutoka nje ili kutimiza asilimia 64 ya mahitaji yake.
Amesema ili kuondoa pengo hili katika mahitaji na kiasi kinachopatikana, ni lazima kukumbatia suluhisho linaloboresha kilimo endelevu cha mpunga, na moja ya suluhisho ni kutambulisha na kutangaza mpunga ulioboreshwa kupitia mbinu bora za kisasa za uzalishaji wa mbegu za mpunga.