Uganda yaomba kuungwa mkono zaidi kimataifa katika suala la wakimbizi
2024-10-25 11:00:59| cri

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada kwa nchi hiyo ili kukabiliana na msukosuko wa wakimbizi unaozidi kuongezeka.

Rais Museveni ametoa wito huo Ikulu mjini Entebbe kwenye mkutano na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Bw. Filippo Grandi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ikulu ya Uganda, Rais Museveni amesema tatizo kubwa lililopo ni mahitaji kama vile chakula na vifaa vya shule, kwa sababu wakimbizi wameleta mahitaji ya ziada.

Rais Museveni amesema Uganda ina sera rafiki kwa wakimbizi ambayo inawavutia wakimbizi kutoka nchi jirani, na haina tatizo na wakimbizi kwani inawapa ulinzi, na haiwalazimishi kuishi makambini.

Kwa mujibu wa UNHCR, Uganda imepokea wakimbizi zaidi milioni 1.7, wengi wao wamekimbia migogoro nchini Sudan, Sudan Kusini, na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).