Zaidi ya watoto milioni 2.8 wa Sudan wakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu huku mzozo wa kivita ukiendelea
2024-10-31 09:53:03| CRI

Mashirika ya kimataifa na mamlaka za Sudan zimesema zaidi ya watoto milioni 2.8 walio chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu huku mizozo ya kivita ikiendelea kuiteketeza nchi hiyo.

Shirika lisilo la kiserikali la kimataifa la Save the Children lilisema kwenye ripoti jana Jumatano kuwa watoto hao, ambao sasa wamekimbia makazi yao kote nchini Sudan, "watakosa mambo muhimu ya utotoni, yakiwemo chanjo, maji safi, huduma ya afya, chakula cha lishe bora, na kujisitiri na joto na baridi kali."

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya nusu ya watu milioni 11 waliokimbia makazi yao, au milioni 5.8, ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 18, huku wengi wao wakiishi katika kambi za wakimbizi, makazi yasiyo rasmi, shule zenye msongamano, au majengo mengine ya umma. Wakati huo huo, mashirika maarufu ya jimbo la kati la Gezira, ambalo linashuhudia mashambulizi yanayoongezeka, yameonya kuwa watoto ndio waathirika wakuu wa wimbi la sasa la ghasia.