Aina za Majengo ya Kitaifa
Majengo ya Kasri
Majengo ya kasri kwa maneno mengine ni majengo ya kifalme. Ni majengo yanayojengwa kwa ajili ya kuimarisha utawala wa wafalme, kutukuza heshima na mamlaka ya wafalme, kukidhi maisha yao ya anasa kiroho na kimali. Kwa hiyo majengo hayo yote yana lengo la kuonesha ufahari.
Kuanzia Enzi ya Qin (221-206 K.K.) nchini China "kasri" lilikuwa ni makazi ya wafalme na jamaa wa wafalme, na ni mahali pa wafalme kushughulikia mambo ya taifa. Ukubwa wa majengo ya kasri uliongezeka kutoka enzi hadi enzi, tofauti yake na majengo mengine ni paa la vigae vyenye rangi ya dhahabu, michoro ya rangi kwenye boriti, ngazi za marumaru, na majengo mengine pembeni mwa kasri. Kasri la Kifalme mjini Beijing ni kielelezo kizuri cha majengo hayo.
Ili kutukuza madaraka ya kifalme na kuonesha kiini cha utawala, majengo ya kifalme yalikuwa yakijengwa kwa ulinganifu kwenye pande mbili za mstari, majengo yaliyojengwa kwenye mstari wa katikati ni makubwa na ya kifahari, na majengo yaliyokuwa kwenye pande mbili za mstari wa katikati ni mafupi na ya kawaida. Kutokana na maadili ya kijamii nchini China ikiwa ni pamoja na kuheshimu mababu, heshima kwa wazee na kuabudu miungu ya ardhi, mbele ya kasri kwenye upande wa kushoto kunajengwa hekalu la kufanyia tambiko kwa mababu, na upande wa kulia hujengwa hekalu la kufanyia tambiko kwa miungu ya ardhini na nafaka. Mpangilio huo unaitwa "mababu upande wa kushoto na miungu upande wa kulia". Na majengo yaliyopo kwenye mstari wa katikati pia yanagawanyika katika sehemu mbili, yaani sehemu ya mbele ni mahali pa kushughulikia mambo ya utawala, na sehemu ya nyuma ni makazi ya wafalme na masuria.
Majengo ya Mahekalu
Mahekalu ni moja ya aina ya majengo ya dini ya Buddha nchini China. Mahekalu nchini China yalianzia India, mahekalu hayo ni ishara ya hali ya ustawi wa dini ya Buddha katika historia, ni majengo yenye thamani kubwa kwa ajili ya uchunguzi na usanii.
Wahenga wa China walizingatia sana ulinganifu wa majengo kwenye kando mbili za mstari wa katikati, hali kadhalika kwenye ujenzi wa mahekalu ya dini ya Buddha. Lakini pia kuna mahekalu yaliyojengwa kama bustani. Aina hizo mbili zinayafanya mahekalu nchini China yawe na taadhima na uzuri wa kimaumbile.
Mpangilio wa ujenzi wa hekalu la kale ni kuwa mbele kuna lango, na baada ya kuingia kwenye lango hilo upande wa kushoto na kulia kuna jumba la kengele na jumba la ngoma, na nyumba kubwa inayokabili lango ni ukumbi wa mungu, ndani ya ukumbi huo kuna sanamu za walinzi wanne wa peponi, nyuma ya ukumbi huo na kuendelea ni ukumbi wa mwasisi wa dini ya Buddha, Sakyamuni. Ukumbi huo ni mkubwa na ni muhimu kabisa kuliko majengo yote ndani ya hekalu. Mahekalu yaliyojengwa kabla ya enzi za Sui (581-618) na Tang (618-907) kwa kawaida hujengwa pagoda mbele ya hekalu au katikati ya ua wa hekalu, na baada ya enzi za Sui na Tang nafasi ya jengo la pagoda imechukuliwa na ukumbi mkubwa, na pagoda hujengwa katika ua mwingine.
Hekalu la Baimasi
Hekalu hili liko katika mji wa Luoyang mkoani Henan, lilijengwa katika Enzi ya Han (206-220 KK.). Hilo ni hekalu la mwanzo kabisa kati ya mahekalu ya dini ya Buddha yaliyojengwa na serikali nchini China. Ujenzi wake ni wa umbo la mstatili kwenye eneo la mita za mraba elfu 40. Ujenzi wa hekalu hilo ulichangia ustawi wa dini ya Buddha nchini China na hata nchi za Asia ya Mashariki na ya Kusini. Hadi sasa hekalu hilo linaendelea kuwa mahali patakatifu kwa waumini wa dini ya Buddha wa nchi nyingi.
Mahekalu katika Mlima Wutaishan
Mlima Wutaishan ni sehemu maarufu ya dini ya Buddha, kuna majengo 58 ya dini ya Buddha mlimani, na kati ya majengo hayo kuna mahekalu ya Nanchansi na Foguangsi yaliyojengwa katika Enzi ya Tang. Hekalu la Nanchansi ni hekalu lenye miaka mingi zaidi kati ya mahekalu yaliyojengwa kwa mbao nchini China. Hekalu hilo lina sifa zote za mahekalu ya enzi mbalimbali nchini China. Kutokana na uhodari wa ujenzi wake, sanamu, picha za ukutani na maandishi ya brashi ya wino, vinasifiwa kuwa ni "maajabu manne".
Hekalu la Xuankongsi
Hekalu hili lastahili kutajwa, kwani ni jengo la ajabu lililojengwa kwenye genge kali mlimani. Hekalu hilo liko umbali wa km. 3.5 kutoka mji mkuu wa wilaya ya Hunyuan, ni jengo lililojengwa kwa mbao. Hekalu hilo lilijengwa katika Enzi ya Wei Kaskazini (386-534), na liliwahi kukarabatiwa katika enzi za Tang, Jin, Ming na Qing. Hekalu hili linakabiliana na mlima Hengshan, na hakuna madaraja ya kupandia, mandhari yake ni ya ajabu katika mlima Hengshan.
Kasri la Potala
Madhehebu ya Lama ni moja ya madhehebu ya dini ya Buddha nchini China, mahekalu ya Lama hujengwa kwa ukumbi mkuu na ukumbi wa kuombea dua. Mahekalu ya madhehebu ya Lama hujengwa mbele ya mlima. Kasri la Potala lililoko mkoani Tibet ni hekalu la madhehebu ya Lama, lilijengwa katika Enzi ya Tang (618-907), na baada ya enzi nyingi kukarabati na kupanua kasri hilo limekuwa na majengo mengi. Kasri hilo lina eneo la mita za mraba elfu 20, kuna kumbi kubwa zaidi ya 20, ndani ya ukumbi mkubwa wa mbele iliwekwa sanamu ya shaba ya mwasisi wa dini ya Buddha, Sakyamuni, iliyopakwa rangi ya dhahabu kwa kulingana sawa na mwili wake alipokuwa na umri wa miaka 12. Kasri la Potala ni jengo lenye mtindo halisi wa ujenzi wa Enzi ya Tang na pia limechukua mitindo ya India na Nepal.
Majengo ya Bustani
Majengo ya bustani nchini China yana historia ndefu, na ni majengo maarufu duniani. Mapema miaka 3000 iliyopita kulikuwa na bustani ya kifalme nchini China. Tokea hapo bustani zilianza kuwepo katika miji mikuu ya enzi mbalimbali na miji mingine mikubwa. Kuna aina nyingi za bustani nchini China ambazo ni muhimu katika mifumo mitatu mikuu ya ujenzi wa bustani duniani.
Bustani nchini China huwa na milima na maji kwa ajili ya kuleta uzuri wa kimaumbile.
Majengo ya bustani nchini China yanagawanyika katika fungu la bustani za kifalme na bustani binafsi. Bustani hizo zilijengwa kwa milima ya bandia na maziwa, maua na miti, nyua za nyumba, na ujia wenye paa na mbao zenye maandishi, bustani yenye mzingira hayo ni kama bustani ya peponi. Bustani nchini China zimegawanyika kwa dhana za aina tatu, yaani dhana za utawala wa kifalme, dhana za mandhari ya kichimbakazi (fairyland) na dhana za mandhari ya kufananisha na hali ya maumbile.
Mandhari ya kichimbakazi yanazingatia kuleta mazingira ya utawa, mazingira ambayo yalifuatwa sana na waumini wa dini ya Dao ya Kichina. Mazingira kama hayo pia yanaonekana katika ujenzi wa mahekalu na bustani za kifalme.
Mandhari ya kufananisha na maumbile yanajengwa kwa kufuata hisia za wenye bustani. Mandhari za namna hiyo zinapatikana zaidi katika bustani za wasomi.
Tofauti kubwa kati ya bustani za Kichina na za Kimagharibi ni kuwa bustani za Kimagharibi zinajengwa kwa kuonesha uzuri wa majengo, na bustani za Kichina zinajengwa kwa nia ya kuonesha uzuri wa mandhari ya kimaumbile na hisia za wenye bustani.
Bustani katika Mji wa Suzhou
Bustani kadhaa mjini Suzhou ziliorodheshwa katika kumbukumbu ya urithi wa dunia mwaka 1997. Bustani katika mji huo zimeingiza sifa zote za bustani nchini China. Bustani hizo zimekuwa na miaka zaidi ya 2000, na zilizobaki sasa ziko 10. Bustani katika mji wa Suzhou nyingi ni ndogo, lakini kutokana na kuwa ndani yake kuna milima ya bandia na maziwa, miti na maua, madaraja madogo na vibanda, bustani hizo zinaonekana mandhari kubwa ya kimaumbile na kufanya watu wahisi wako kwenye mazingira ya utamaduni mkubwa.
Bustani ya Kifalme Yuanmingyuan
Bustani hiyo ya kifalme ilikuwa na mchanganyiko wa mitindo ya Kichina na Kimagharibi. Hii ilikuwa ni bustani nzuri kuliko zote nchini China. Lakini mwaka 1860 bustani hiyo iliteketezwa na muungano wa wavamizi wa Uingereza na Ufaransa. Hivi sasa watu wanaweza tu kukisia jinsi ilivyokuwa nzuri kwa kuangali magofu yake.
Bustani ya Kifalme ya Yuanmingyuan iko katika kitongoji cha Beijing upande wa kaskazini magharibi. Bustani hiyo licha ya kuwa bustani nzuri kuliko bustani nyingine za kifalme pia imewahi kujulikana hata barani Ulaya kutokana na maelezo ya barua za wamisionari na ilikuwa na athari kwa ujenzi wa bustani za Ulaya.
Ujenzi wa Makaburi
Ujenzi wa makaburi ni sehemu muhimu katika ujenzi wa China ya kale. Kutokana na imani ya wahenga wa China kuwa roho ya marehemu inadumu milele, mazishi yalikuwa yakitiliwa maanani sana, kwa hiyo watu walikuwa makini sana katika ujenzi wa makaburi. Katika historia ndefu nchini China ujenzi wa makaburi ulipata maendeleo makubwa na makaburi mengi maarufu ya wafalme na malkia yalijengwa. Kutokana na jinsi muda ulivyokuwa ukipita, ujenzi wa makaburi ulichanganywa na sanaa za uchoraji na uchongaji wa sanamu, na kuyafanya makaburi yawe na mkusanyiko wa sanaa za aina nyingi.
Ujenzi wa makaburi nchini China ni mkubwa na wenye majengo mengi. Kwa kawaida ujenzi huo hutumia vizuri sura ya kimaumbile ya ardhi kwenye milima, ingawa pia kulikuwa na makaburi yaliyojengwa katika sehemu za tambarare. Kwa kawaida mpangilio wa majengo ya makaburi huwa na uzio unaozunguka sehemu ya kaburi, na kila upande kuna mlango mmoja, na kwenye kila kona ya uzio kuna jumba la ghorofa, mbele ya kaburi kuna barabara na kwenye pande mbili za barabara kuna sanamu kubwa za mawe za wanyamapori na askari walinzi, ndani ya uzio huo imepandwa misonobari mingi, mazingira hayo yaliwafanya watu kuwa na heshima kubwa kwa marehemu katika hali ya ukimya kabisa.
Kaburi la Mfalme Qinshihuang
Kaburi la mfalme Qinshihuang (259K.K.-210K.K.) liko nje ya mji wa Xi'an mkoani Shanxi upande wa kaskazini mwa Mlima Lishan, hilo ni moja ya makaburi maarufu nchini China. Kaburi hilo lilijengwa miaka 2000 iliyopita. Sanamu za askari na farasi zinazosifiwa kuwa ni moja ya "maajabu nane duniani" ni "walinzi wa kaburi" hilo. Sanamu hizo ziliwekwa na UNESCO katika orodha ya urithi wa dunia mwaka 1987. Kamati ya Urithi wa Dunia ilisema, "Sanamu zenye sura mbalimbali za askari, farasi na mikokoteni ya kivita iliyoko pembezoni mwa kaburi la mfalme Qinshihuang ni sanaa adimu aidha iwe katika zama hizi au za kale, zina thamani kubwa za kihistoria.
Sehemu iliyo karibu na mji wa Xi'an lina makaburi mengi ya wafalme, licha ya kaburi la mfalme Qinshihuang, kuna makaburi 11 ya wafalme wa Enzi ya Han Magharibi (206 K.K.-220) na 18 ya wafalme wa Enzi ya Tang (618-907).
Makaburi ya Wafalme wa Enzi ya Ming na Qing
Makaburi ya wafalme wa Enzi ya Ming na Qing ni makaburi ya wafalme yaliyohifadhiwa kikamilifu nchini China.
Makaburi hayo yako katika kitongoji cha Changping nje ya Beijing chini ya mlima Tianshoushan, wafalme 13 walizikwa huko baada ya mji mkuu wa Enzi ya Ming kuhamishwa kwenye mji wa Beijing kutoka mji wa Nanjing. Makaburi hayo yako katika bonde lililozungukwa na milima kwa pande tatu. Kwenye mteremko wa mlima yalipangwa makaburi hayo 13, eneo la makaburi ni kilomita 40 za mraba. Katika sehemu hiyo wamezikwa wafalme 13, malkia 23 na wake wenzao, watoto na mabinti wa wafalme.
Makaburi ya wafalme 13 wa Enzi ya Ming yalijengwa kwa adhama kubwa na penye mandhari nzuri, ni fungu kamili la makaburi ya wafalme nchini China. Kati ya makaburi hayo, kaburi la Changling yaani kaburi la mfalme wa tatu, Zhuli, na kaburi la Ding yaani kaburi la mfalme wa 14 wa enzi ya Ming, Zhuyi, ni makaburi makubwa zaidi. Baada ya kufukuliwa, watu wamegundua kuwa ukumbi wa ardhini bado ni madhubuti ambao ulijengwa kwa mawe wenye nusu duara ya paa kwa mawe, pembeni mwa ukumbi huo kuna mitaro ya maji, na tao la mawe halikutitia, ikionesha ufundi mkubwa wa ujenzi wa ukumbi huo katika China ya kale.
Sehemu ya mashariki nje ya Beijing kuna eneo la kilomita za mraba 78 za makaburi ya wafalme wa Enzi ya Qing (1616-1991), sehemu ya makaburi ni kilomita za mraba 78, wafalme watano na malkia 14 wa Enzi ya Qing walizikwa huko. Huko makaburi yote yalijengwa kwa makini na ufahari.
Makazi ya Watu
China ni nchi kubwa yenye sehemu tofauti na utamaduni tofauti. Kutokana na hali hiyo makazi ya watu pia yanatofautiana.
Katika sehemu wanazokaa watu wa kabila la Han, makazi ya watu hujengwa kwa nyumba za chini zenye nyua za mraba, mfano wa ujenzi huo ni makazi yaliyopo mjini Beijing. Nyumba za chini zenye nyua za mraba mjini Beijing zimegawanyika kuwa ua wa mbele na ua wa nyuma. Nyumba iliyopo katikati ua wa mbele na ua wa nyuma ni ya heshima kabisa, ni mahali pa kufanyia sherehe za familia, na kupokelea wageni wa heshima. Nyumba zote pembeni mwa ua wa mbele na ua wa nyuma zinaelekea katikati ya ua na zinaunganishwa kwa ujia wenye paa. Kuishi katika nyumba kama hizi ni starehe na kwa sababu ya kuishi pamoja katika nyumba hizo uhusiano wa jamaa ni wa karibu sana. Nyumba za aina hiyo zipo katika sehemu za kaskazini, na kaskazini mashariki za China.
Nyumba za Ghorofa za Udongo
Majumba ya ghorofa ya aina hiyo yanajengwa zaidi katika sehemu za kusini za China, umbo la nyumba linakuwa la duara, mraba au la yai, mithili ya ngome. Katikati ya jumba hilo ni kiwanja ambacho kuna kisima na ghala la nafaka. Milango ya nyumba ikifungwa kwa ajili ya kuzuia wezi au katika siku za vita, watu wanaoishi ndani ya nyumba hiyo wanaweza kukaa humo bila wasiwasi wa kukosa maji wala chakula kwa miezi kadhaa. Kwa kawaida nyumba kama hizo huwa na ghorofa tatu au nne.
Nyumba za ghorofa za udongo zinajengwa kwa mchanganyiko wa udongo, kokoto, mchanga na mbao, katika siku za majira ya baridi, ndani nyumba kunakuwa na joto, na katika siku za majira ya joto ndani ya nyumba kuwa na baridi, na tena ni madhubuti hata likitokea tetemeko la ardhi.
Makazi ya Watu wa Makabila Madogo Madogo
Makazi ya watu wa makabila madogo madogo pia yako aina nyingi. Makazi ya kabila la Uygur mkoani Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, yanajengwa kwa paa lililo bapa, kuta za udongo na ghorofa moja au mbili, na kuna ua mbele ya nyumba; Makazi ya kabila la Watibet yanajengwa kama ngome, kuta za mawe kwa nje na mbao kwa ndani na paa lililo bapa; Watu wa kabila la Wamongolia ni wafugaji, wanaishi katika mahema ambayo ni rahisi kuyahamisha kufuata malisho ya mifugo; Watu wa makabila madogo madogo katika sehemu ya kusini magharibi mwa China wanaishi katika nyumba zilizojengwa milimani karibu na maji, ghorofani wanaishi watu, na chini inaishi mifugo au kutunza vitu mbalimbali. Majumba hayo hujengwa kwa mianzi na kusimamishwa kwa nguzo bila kuwa na msingi ardhini.
Mapango na Makazi katika Miji ya Kale Kaskazini mwa China
China ni nchi kubwa yenye makabila mengi, kwa hiyo makazi pia ni ya aina nyingi. Makazi katika sehemu za mwanzo na katikati ya Mto Huanghe, mengi zaidi ni ya mapango, makazi hayo yako katika mikoa ya Shan'xi, Gansu, Henan na Shanxi. Wakazi wa sehemu hizo wanachimba mapango kwenye milima ya udongo na familia moja huwa na mapango kadhaa yanayounganishwa kwa ndani. Kwa ndani mapango hujengwa kwa matofali. Mapango hayo hayashiki moto, yanazuia kelele, na huwa na baridi wakati wa majira ya joto na joto katika majira ya baridi, na hayatumii ardhi ya kilimo.
Nchini China kuna miji ya kale ambayo mpaka sasa bado iko vilevile. Ndani ya miji hiyo kuna makazi mengi ya kale. Kati ya miji hiyo, mji wa Pingyao, mkoani Shanxi, kaskazini mwa China, na mji wa Lijing, mkoani Yunan kusini mwa China, imeorodheshwa katika kumbukumbu za urithi wa dunia mwaka 1998.
Mji wa Pingyao ni mji kamili uliobaki tangu Enzi ya Ming na Qing, ni mfano wa ujenzi wa miji ya kale katika sehemu ya kati ya China. Hadi sasa mji huo bado upo kama ulivyokuwa zamani. Kuta zake za mji, barabara, makazi, maduka na mahekalu bado yapo. Ni sampuli kwa ajili ya utafiti wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, mambo ya kijeshi, ujenzi na sanaa katika histroria ya China.
Mji wa Lijiang ni mji uliokuwepo toka Enzi ya Song Kusini (1127-1279). Ujenzi wa mji huo ni mchanganyiko wa mitindo ya kabila la Wanaxi na mitindo ya nchi za nje. Kutokana kutoathiriwa na itikadi ya kimwinyi iliyotawala sehemu za ndani za China, barabara za mjini hazikupangwa kwa utaratibu, wala hakuna kuta za mji. Ziwa la Heilong ni chanzo cha maji, mito midogo mingi inaanzia kwenye ziwa hilo na kupeleka maji kwenye makazi, kwa hiyo ndani ya mji mito midogo inaonekana kila mahali, na kwenye kingo za mito hiyo kuna miti mingi.
|