Washairi Wakubwa katika China na Kale
Mwandishi Su Shi
Su Shi alizaliwa mwaka 1037 na kufa mwaka 1101, alikuwa mwenyeji wa Mkoa Sichuan. Baba yake alikuwa mwanafasihi, kuokana na kuathiriwa na baba yake, toka alipokuwa mtoto alikuwa na ari ya kupigania mustakbali mzuri wa maisha yake. Baada ya yeye kushika wadhifa alikuwa mtetezi wa kufanya mageuzi ili alitawale taifa kwa amani. Alipokuwa ofisa wa kisehemu na diwani wa mfalme alikuwa mwanamageuzi mwenye juhudi akijaribu kuondoa sera zenye madhara na kutetea zile zenye maendeleo.
Kutokana na tabia yake ya kudhihirisha wazi kila kitu moyoni mwake na kuthubutu kusema kinaganaga mbele ya mfalme, mwishowe alikuwa msingiziwa katika mivutano kati ya vikundi vya madiwani wa mfalme. Mara kadhaa alipewa adhabu ya kufukuziwa mbali, na kila mara mazingira ya kuishi yalikuwa mabaya zaidi. Kutokana na ugumu wa maisha alikuwa amepata falsafa ya Confucius, ya dini ya Buddha na ya dini ya Dao akawa mtu mwenye moyo mpana wa kujiliwaza kutokana na maisha yake magumu na huku alikuwa mtu mwenye matumaini mema ya binadamu na kuyapigania katika maisha yake.
Hulka ya Su Shi ya unyoofu bila kuficha lolote moyoni ilisifiwa sana katika kipindi cha mwisho cha jamii ya umwinyi nchini China na iliathiri wasomi kwa miaka 800.
Mshairi Du Fu
Katika historia ya fasihi ya China watu hutaja washairi wawili wakubwa Li Bai na Du Fu kuwa ni wawakilishi wa mafanikio makubwa ya uashairi katika Enzi ya Tang (618-907).
Du Fu alizaliwa mwaka 712, alikuwa ni mjukuu wa mshairi mashuhuri Du Shenyan. Du Fu alikuwa mtoto mwenye kipaji kisicho cha kawaida. Toka utotoni mwake alikuwa na hamu ya kujifunza na alipokuwa na umri wa miaka 7 alianza kutunga mashairi. Baada ya kuwa mtu mzima alikuwa hodari wa kuchora picha, kupanda farasi na kucheza kitara. Tokea alipokuwa na umri wa miaka 19 alianza kutembelea huku na huko kwenye mandhari nzuri ya mito na milima na alipata kuona mengi, wakati huo kilikuwa ni kipindi cha ustawi kabisa cha Enzi ya Tang.
Kama walivyokuwa wasomi wengi wengine wa China, Du Fu pia alitamani kuwa na wadhifa fulani katika utawala wa kifalme, mara nyingi alikuwa anawasifu watu wenye madaraka na matajiri lakini hakupata chochote. Alipokuwa mtu wa makamo aliishi maisha ya kimaskini katika mji mkuu wa Enzi ya Tang, Chang An, na alishuhudia hali ya kusikitisha ya watu maskini kufa kwa njaa na baridi huku matajiri wakiishi maisha ya anasa, aliandika kifungu kinachojulikana kwa wote hadi leo, "Nyama na pombe zaoza nyumbani kwa matajiri, watu maskini wanakufa mitaani". Maisha yake magumu yalimfanya aelewe kwa kina ufisadi wa watawala na janga la watu maskini, na kumfanya awe mshairi anayehangaikia sana hali ya taifa na wananchi.
Mwaka 755 Du Fu alipokuwa na umri wa miaka 43 alipata wadhifa, lakini baada ya mwezi mmoja vita vilizuka na kuendelea kwa muda mrefu. Katika kipindi hiki Du Fu alizurura zurura akiwa na maisha magumu na alikuwa ametambua vema jamii aliyoishi na aliandika mashairi mengi maarufu.
Mwaka 759 alikuwa amekata tamaa kabisa kuhusu siasa, aliacha wadhifa wake. Wakati huo kulitokea ukame na maisha yake yalikuwa ya kimaskini kabisa na hata alishindwa kuendelea na maisha yake, aliwaongoza jamaa yake kwenda kwenye mji uliopo katika sehemu ya kusini magharibi ya China. Kutokana na msaawa wa marafiki zake aliishi kwa miaka minne bila kuwasiliana na wengine, wakati huo aliandika shairi maarufu la kuelezea maisha yake magumu la "Nyumba Iliyoezeuliwa paa na Upepo", akionesha matumaini yake ya kukubali kulala mitaani kama angeweza kuwapatia watu wote nyumba ili wajihifadhi kwenye ya kuhifadhi kwenye joto.
Du Fu alifariki mwaka 770 alipokuwa na umri wa miaka 59 kutokana na umaskini na ugonjwa akiwa katika safari ya kuzurura. Mashairi ya Du Fu yaliyobaki sasa yako 1400, kwa kina yameonesha miaka 20 hali ya jamii yenye vurugu ya vita, kutoka ustawi hadi kuporomoka kwa uchumi katika Enzi ya Tang.
Mshairi Li Bai
Li Bai alizaliwa mwaka 701 na kufariki dunia mwaka 762, alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Gansu wa leo. Hadi sasa haijafahamika kama alizaliwa katika ukoo gani, lakini kutokana na mashairi yake tunaweza kufahamu kuwa yeye alizaliwa katika ukoo wenye hali nzuri kiuchumi na kiutamaduni. Tokea alipokuwa mtoto alipenda kusoma na alisoma vitabu vingi. Tangu alipokuwa na miaka 20 alianza kutembelea kila mahali ili kuona mengi. Kutokana na elimu yake kubwa na akili yake timamu, alifanikiwa sana katika uandishi wa mashairi. Ingawa wakati huo hali ya uchapaji na mawasiliano ilikuwa duni, lakini kupitia maingiliano ya wasomi jina lake lilijulikana sana.
Kusoma ili kujipatia nyadhifa ni tumaini la wasomi wote katika enzi za kale za China. Li Bai alipokuwa kijana alikuwa na tumaini kubwa la kupata wadhifa, kutokana na lengo hilo alikwenda mji mkuu wa Enzi ya Tang, Changan. Kutokana umaarufu wake na kupendekezwa na wasomi, mwaka 742 alichaguliwa kuwa afisa katika kasri la mfalme. Huu ulikuwa ni wakati mzuri kabisa maishani mwake.
Li Bai alikuwa ni mtu mwenye kiburi, alikuwa na malalamiko mengi kuhusu ufisadi na alitamani kuthaminiwa zaidi na mfalme, ili aoneshe uhodari wake katika mambo ya siasa, lakini mfalme alimchukulia kama ni mshairi aliyetumiwa tu wakati mfalme anapokuwa na haja naye. Li Bai alikata tamaa, na aliondoka mji mkuu Changan na kuanza tena maisha ya kutembea tembea kila mahali akiwa anajifariji kwa kunywa pombe na kuandika mashairi.
Mashairi ya Li Bai yaliyobaki hadi sasa ni zaidi ya 900.
Mashairi Yaliyopamba Moto katika Enzi ya Tang
Enzi ya Tang ni kipindi muhimu katika historia ya China. Katika kipindi hicho uchumi ulistawi, jamii ilikuwa tulivu, utamaduni na sanaa viliendelea kwa haraka na hasa mashairi yalikuwa yamepamba moto. Kutunga mashairi kulikuwa ni maisha muhimu ya wasomi katika Enzi ya Tang. Kitabu kiitwacho "Mkusanyiko wa Mashairi ya Enzi ya Tang" kimekusanya mashairi karibu elfu 50 yaliyoandikwa na washairi zaidi ya elfu mbili na mia tatu.
Maendeleo ya mashairi ya Enzi ya Tang yanaweza kugawanyika katika vipindi vinne vya enzi hiyo, navyo ni kipindi cha mwanzo, kipindi cha ustawi, kipindi cha katikati na kipindi cha mwisho.
Kipindi cha mwanzo (618—712). Katika kipindi hiki waliibuka "washairi hodari wanne", nao ni Wang Bo, Yang Jong, Lu Jielin na Luo Binwang ambao waliweka kanuni za mashairi ya kale yenye mistari maalumu na kila mstari uwe na maneno maalumu yaani maneno matano au maneno saba. Kutokana na juhudi zao mashairi hayakuwa ya burudani tena ndani ya kasri la kifalme, bali yamekuwa yakieleza maisha halisi ya wananchi.
Kati ya mwaka 712 hadi mwaka 762 kilikuwa ni kipindi cha ustawi cha Enzi ya Tang. Katika kipindi hiki uandishi wa mashairi ulipamba moto. Kulikuwa na mada nyingi za mashairi zikielezea uzuri wa maumbile, kusifu mashujaa na kueleza hisia za masikitiko. Washairi walikuwa wakiandika mashairi katika mazingira ya uhuru na kukifanya kipindi hiki kifikie kilele cha mashairi katika historia ya China.
Katika kipindi hiki cha ustawi cha Enzi ya Tang, washairi wakubwa walikuwa ni Li Bai, Du Fu, Wang Wei, Meng Haoran, Gao Shi na Cen Can. Kati ya hao Li Bai na Du Fu ndio wawakilishi wa washairi wa kipindi hiki, mashairi yao yameathiri sana mashairi ya hapo baadaye.
Katika kipindi cha Katikati cha Enzi ya Tang (762—872) washairi walio maarufu zaidi ni Bai Juyi, Yuan Zhen na Li He. Bai Juyi alikuwa hodari wa kuandika mashairi ya kudhihaki utawala wa kutoza kodi kubwa, kupinga vita na kuwaponda matajiri wenye madaraka, na alijitahidi kutumia lugha rahisi. Mashairi yaliwapendeza sana wasomaji.
Li He alikuwa na maisha mafupi, aliishi zaidi ya miaka 20 tu. kutokana na kuwa maisha yake yalikuwa magumu na tumaini lake liligongwa mwamba, mashairi yake yalijaa huzuni.
Kipindi cha mwisho cha Enzi ya Tang (827—859) ni kipindi ambapo cha washairi Li Shangyin na Du Mu walikuwa katika kilele cha kuandika mashairi. Mashairi ya Du Mu, mengi yalikuwa yakionesha nia yake ya kisiasa, na mashairi ya Li Shangyin mengi yalikuwa yakionesha masikitiko na simanzi kutokana na usumbufu wake alipokuwa na wadhifa.
Mshairi wa kueleza mandhari ya maumbile Tao Yuanming
Tao Yuanming pia anaitwa Tao Qian, alikuwa ni mshairi wa kueleza mandhari ya maumbile. Alikuwa mtu wa kuridhika na maisha yake ya umaskini, mwenye hulka ya unyoofu, wasomi wa baadaye walimsifu sana.
Baba wa babu wa Yuan Mingyuan alikuwa ni mwanzilishi wa Enzi ya Jin Mashariki, babu yake na baba yake wote walikuwa ni maofisa. Tao Yuanming alipokuwa na umri wa miaka minane baba yake alifariki, hali ya familia ikawa duni. Alipokuwa mtoto alikuwa na tumaini kubwa la kuwa ofisa na kutoa mchango katika mambo ya kisiasa.
Lakini Enzi ya Jin Mashariki kilikuwa ni kipindi cha vurugu, migogoro kati ya maofisa na ufisadi vilikithiri katika kasri la mfalme. Ilikuwa muda mfupi baada ya Tao Yuanming kuwa na wadhifa alipokuwa na umri wa miaka 29, alijiachisha kazi na kurudi nyumbani kutokana na kutoweza kuvumilia ufisadi huo.
Maisha ya Tao Yuanming yalikuwa mabaya siku hadi siku, na hata alishindwa kuwalisha jamaa zake kwa kulima, ilimpasa ajitafutie wadhifa, na alipokuwa na umri wa miaka 41 alikuwa ofisa wa wilaya. Lakini kutokana na hulka yake ya kuchukia matajiri na kujinyenyekea, alikuwa madarakani kwa siku 80 tu alijiachisha kazi. Tokea hapo alikuwa ameacha kabisa wadhifa na kuishi kwa kutegemea kilimo.
Maisha yake ya kilimo yalikuwa mabaya sana, alipokuwa na umri wa miaka 44 nyumba yake iliungua, maisha yalikuwa magumu zaidi. "Kukaa na njaa katika siku za joto, na kulala bila mfarishi katika siku za baridi" ni beti iliyoeleza hasa umaskini kwenye maisha yake. Lakini alikuwa na moyo mtulivu kuvumilia umaskini huo. Katika kipindi hicho aliandika mashairi mengi ya kueleza mandhari ya vijijini. Kutokana na kalamu yake, kwa mara ya kwanza maisha ya wakulima na mandhari ya vijijini ilikuwa mada muhimu katika maandishi.
Maisha ya uzeeni ya Tao Yuanming yalikuwa ya kusikitisha sana, hata mara nyingne alikuwa anaomba, hata hivyo alipokuwa maskini sana alikataa wadhifa kwa mara nyingine tena. Insha aliyoandika uzeeni "Matembezi katika Kijiji cha Taohuayuan" inajulikana kwa wote. Katika makala hiyo alieleza mvuvi mmoja aliyepotea njia aliingia katika kijiji hicho aligundua baadhi ya watu wanaoishi katika kijiji hicho, watu ambao kizazi kwa kizazi waliishi huko kwa ajili ya kukwepa vurugu za vita, walikuwa hawajui dunia ilivyo nje ya kijiji hicho, wote walikuwa ni watu wenye juhudi za kazi na waaminifu, wakiishi maisha ya utulivu bila wasiwasi. Maisha ya watu katika kijiji cha Taohuayuan yaliwakilisha matumaini mema ya mshairi Tao Yuanming ya amani badala ya jamii iliyojaa vurugu za vita.
Mashairi na makala za Tao Yuanmin zilizobaki ziko zaidi ya mia moja tu, lakini nafasi ya mshairi huyo katika historia ya fasihi ya Kichina ni muhimu sana.
Qu Yuan na Mashairi Yake
Qu Yuan ni mshairi anayependwa na kuheshimiwa sana na Wachina. Mshairi huyo aliishi katika Kipindi cha Madola Yaliyopigana Vita (475 K.K.—221 K.K.). Katika kipindi hicho madola madogo madogo yalikuwa mengi, na yalipigana vita miaka hadi miaka. Kati ya madola hayo, Dola la Qin na Chu yalikuwa na nguvu zaidi, madola mengine yalikuwa yakifuata madola hayo mawili.
Qu Yuan alikuwa mtu wa tabaka la matajiri na alikuwa ofisa mwandamizi katika serikali. Alikuwa mwenye elimu nyingi na alikuwa hodari wa mambo ya diplomasia, kwa hiyo alipendwa na kuaminiwa sana na mfalme wa Dola la Chu. Katika kipindi hicho kila mfalme alikuwa anawakusanya watu wenye elimu kwa unyekekevu, na hali hiyo ilishamiri sana katika kila dola. Wasomi wengi wakubwa walitembeatembea kati ya madola ili watimize malengo yao ya kisiasa. Lakini Qu Yuan alikuwa kinyume na hali hiyo, aling'ang'ania kukaa nchini Chu akitumai kumsaidia mfalme wake kwa elimu yake na kumwelimisha mfalme awe fikra za kimaendeleo na kulifanya Dola la Chu liwe la nguvu na ustawi. Lakini bahati mbaya aligongana sana na kundi la matajiri katika mambo ya ndani na nje, na zaidi ya hayo alisingiziwa na wengine, hivyo alipuuzwa na mfalme wa Chu. Tokea hapo hadhi ya Dola la Chu ilishuka na nguvu zilififia. Mwaka 278 K.K. jeshi la Dola la Qin lilivamia Dola la Chu na liliteka mji mkuu wa Dola la Chu. Taifa liliporomoka, na Qu Yuan alijitumbukiza mtoni kutokana na huzuni na hasira.
Maandishi aliyowaachia watu wa baadaye ni utenzi wake Li Sao (uchungu wa moyo). Utenzi huu kwa kutumia mifano ya mambo ya kale alitamani mfalme wa Chu angekuwa kama wafalme werevu wa kale Yao, Shun na Yu waliothamani watu wenye elimu na hekima, na kwa uadilifu na maadili kuendesha utawala na kuunganisha madola mengine kupambana na Dola la Qin.
Kitabu cha Kwanza cha Mkusanyiko wa Mashairi
"Mashairi ya Kale"
Katika karne ya saba K.K. kitabu cha kwanza kabisa cha mkusanyiko wa mashairi "Mashairi ya Kale" kiliandikwa. Ndani ya kitabu hicho yalikusanywa mashairi ya aina mbalimbali ya masimulizi ya matukio, mapenzi, vita na nyimbo za kusifu mambo fulani. Mashairi hayo hayakuandikwa na mtu mmoja. Kitabu hicho kilikusanya mashairi 305 yaliyokuwa katika miaka mia tano.
Mashairi katika kitabu hicho hapo awali yalikuwa kwa ajili ya matumizi ya kuimbwa katika sherehe, burudani na kuonesha fikra za kisiasa, na baadaye yalikuwa masomo ya watu wa tabaka la matajiri. Kusoma kitabu hicho kulikuwa dalili ya elimu ya juu. Masomo hayo yalisaidia sana lugha katika maingiliano ya kijamii, watu walikuwa wakitumia beti fulani za mashairi kueleza maana yake bila kusema moja kwa moja. Confucius aliwahi kusema, "bila kusoma 'Mashairi ya Kale' mtu hawezi kuongea", alisifu sana kitabu hicho.
Kwa muhtasari, "Mashairi ya Kale" ni mwanzo wa fasihi kubwa ya China, ni dalili ya ustawi wa fasihi. Mashairi yake yalihusika na pande mbalimbali, na lugha yake ni tegemeo muhimu katika utafiti wa lugha ya Kichina katika kipindi cha karne ya 11 K.K. hadi karne ya sita K.K.
|