Opera za sehemu mbalimbali za China
Opera ya Huangmei
Katika karne ya 18, opera ya Huangmei ilitokea katika mikoa ya Anhui, Hubei na Jiangxi, na kufikia karne ya 19 opera hiyo imekuwa aina moja muhimu kati ya opera za Kichina.
Opera ya Huangmei huoneshwa kwa kuimba na kucheza, na kueleza matukio katika maisha ya raia. Michezo maarufu inayooneshwa kwa opera ya Huangmei ni "kukutana njiani", "wanandoa wafurahia taa" n.k.
Opera ya Kun
Opera ya Kun inaimbwa kwa lafudhi ya sehemu ya kusini ya China. Aina hiyo ya ilianzia mkoani Jiangsu katika sehemu ya mlima Kun, kwa hiyo inaitwa opera ya Kun .
Opera hiyo ilifika kileleni katika Enzi ya Ming na Qing. Katika kipindi hicho michezo iliyotungwa kwa ajili ya opera hiyo ilikuwa mingi, na walitokea wachezaji wengi hodari.
Lugha inayotumika katika opera hiyo ni nzuri sana, bila kuangalia opera yenyewe, hata ukisoma maandishi ya michezo utafurahia lugha yake nzuri.
Opera ya aina hiyo huoneshwa kwa kuimba na kucheza kwa kushirikiana na bendi. Maendeleo ya opera ya Kun yaliathiri sana opera za aina nyingine kama za Chuan , Xiang , Yue , na Huangmei . Watu husema, opera ya Kun ni asili ya opera zote nchini China.
Opera ya Yu
Opera ya Yu imeenea sana katika mikoa ya Henan, Hebei, Shandong, Shanxi, Hubei, Ningxia, Qinghai na Xinjiang, ni moja kati ya opera muhimu nchini China.
Opera hiyo ilianza mwishoni mwa Enzi ya Ming na mwanzoni mwa Enzi ya Qing.
Bendi ya opera hiyo huwa na ala za muziki za erhu , sanxian , pipa , filimbi, sheng na tarumbeta.
Opera hiyo huchezwa kwa kuimba, inaeleza wazi hisia za mtu, na michezo inayooneshwa kwa opera hiyo huwa ni maisha ya kila siku ya raia, ikionesha hadithi tokea mwanzo mpaka mwisho.
Kabla ya mwaka 1927 opera hiyo ilikuwa haina wachezaji wanawake. Baadaye walitokea wachezaji hodari na maarufu sana kama Chang Xiangyu, Chen Suzhen, Ma Jinfeng, Yan Lipin, Cui Lantian ambao wanajulikana kote nchini China.
Kuna michezo ya jadi ya opera ya Yu zaidi ya 1000, na mingi inaeleza mambo ya historia. Baada ya Jamhuri ya Watu wa China kuasisiwa, michezo inayoeleza maisha ya zama za leo ilianza kutokea. Hivi sasa ingawa opera hiyo inavutia sana watu wengi, lakini imekumbwa na matatizo, kwamba idadi ya watazamaji imepungua, vikundi vya opera hiyo vina matatizo ya kifedha, na wachezaji wanapungua.
|