2: Siasa

Vyama vya China

Chama cha kikomunisti cha China

Chama cha kikomunisti cha China ni chama cha watangulizi wa tabaka la wafanyakazi wa China, pia ni chama cha watangulizi wa wananchi wa China na taifa la China. Chama hicho ni kiini cha uongozi wa jitihada za ujenzi wa mambo ya ujamaa wenye umaalum wa kichina, ambacho kinawakilisha matakwa ya maendeleo ya nguvukazi ya kisasa ya China, kuwakilisha mwelekeo wa kusonga mbele wa utamaduni wa kisasa wa China na kuwakilisha maslahi ya kimsingi ya wanachi wengi kabisa wa China.

Tumainio kubwa kabisa na lengo la mwisho la Chama cha kikomunisti cha China ni kutimiza ukomunisti. Katiba ya chama hicho inaeza kuwa, dira ya vitendo vya Chama cha kikomunisti cha China ni Umax-Lenin, Fikra Mao Zedong, Nadharia ya Deng Xiaoping na wazo muhimu la "Uwakilishi mtatu".

Chama cha kikomunsti cha China kilizaliwa mwezi Julai mwaka 1921. Toka mwaka 1921 hadi 1949, chama hiki kiliwaongoza wananchi wa China katika kufanya mapambano magumu, na kupindua utawala wa ubeberu, umwinyi na ubepari wa utawala msonge, hatimaye kuanzisha Jamhuri ya Watu wa China. Baada ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, Chama cha kikomunsti cha China kiliwaongoza wananchi wa makabila mbalimbali wa nchi nzima katika kulinda uhuru na usalama wa nchi, kufanikiwa kuiwezesha jamii ya China ibadilike kuwa jamii ya ujamaa badala ya jamii ya demokrasia mpya, na kuanzisha ujenzi mkubwa wa ujamaa kwa kufuata mipango, na kuyafanya mambo ya uchumi na utamaduni ya China yapate maendeleo makubwa sana ambayo hayakupatikana katika historia.

Baada ya kukamilisha kimsingi mageuzi ya kiujamaa ya mfumo wa umilikaji wa binafsi wa raslimali za uzalishaji mwaka 1956, kutokana na ukosefu wa uzoefu, Chama cha kikomunisti cha China kiliwahi kufanya makosa kadhaa katika mchakato wa kuongoza ujenzi wa ujamaa; na makosa makubwa yaliyowahi kufanyika ni "mapinduzi makubwa ya utamaduni" kote nchini kwa muda mrefu, tokea mwaka 1966 hadi 1976.

Mwezi Oktoba mwaka 1976, "mapinduzi makubwa ya utamaduni" yalikomeshwa, China ikaingia katika kipindi kipya cha maendeleo ya historia. Baada ya kufanyika kwa mkutano wa 3 wa wajumbe wote wa Kamati kuu ya 11 ya Chama cha kikomunisti cha China mwishoni mwa mwaka 1978, mabadiliko makubwa yenye umuhimu mkubwa yalipatikana tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Kuanzia mwaka 1979, Chama cha kikomunisti cha China kilitekeleza sera iliyopendekezwa na Deng Xiaoping kuhusu kufanya mageuzi na kuzifungulia mlango nchi za nje. Tokea sera hiyo ianze kutekelezwa, mafanikio makubwa ya kuvutia dunia nzima yalipatikana katika maendeleo ya uchumi na jamii ya China, ambapo sura ya nchi ilipata mabadiliko makubwa kabisa, kipindi hiki ni kipindi chenye hali nzuri kabisa tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, vilevile ni kipindi ambacho wananchi walipata manufaa makubwa kabisa.

Chama cha kikomunisti cha China kinatetea kufanya juhudi za kuendeleza uhusiano na nchi za nje na kufanya juhudi za kujipatia mazingira ya kimataifa yanayosaidia mageuzi na ufunguaji mlango na ujenzi wa mambo ya kisasa ya China. Katika mambo ya kimataifa, Chama cha kikomunisti cha China kinashikilia sera ya kidiplomasia ya amani ya kujitawala na kujiamulia mambo, kulinda uhuru na mamlaka ya nchi ya China, kupinga umwamba na siasa ya mabavu, kulinda amani ya dunia na kusukuma mbele maendeleo ya binadamu; kuendeleza uhusiano na nchi mbalimbali duniani kwa msingi wa kanuni tano za kuheshimu mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi, kutoshambuliana, kutoingiliana mambo ya ndani, kuwa na usawa na kunufaishana, na kuishi pamoja kwa amani. Chama cha kikomunisti cha China kimeanzisha na kuendeleza uhusiano wa kirafiki na vyama vya nchi mbalimbali kwa kufuata kanuni nne za kujitawala na kujiamulia, kuwa na usawa kabisa, kuheshimiana na kutoingiliana mambo ya ndani. Hivi sasa Chama cha kikomunisti cha China kimedumisha mawasiliano ya kirafiki na vyama zaidi ya 300 vya nchi zaidi ya 120 duniani.

Chama cha kikomunisti cha China ni umoja unaojumuika kwa kufuata mwongozo na katiba yake na utaratibu wa utawala wa kidemokasia. "Katiba ya Chama cha kikomunisti cha China" inaeleza kuwa, watangulizi wa wafanyakazi, wakulima wanajeshi, wasomi na wengine wa jamii, yeyote aliyetimia umri wa miaka 18, anayetambua mwongozo na katiba ya chama, anayependa kujiunga na jumuiya ya chama na kufanya kazi kwa bidii ndani yake, anayetekeleza maazimio ya chama na kutoa ada ya mwanachama kwa wakati, anaweza kutoa ombi la kujiunga na Chama cha kikomunisti cha China.

Vyombo vya kamati kuu ya chama ni pamoja na Bunge la umma la China, Kamati kuu ya chama, Ofisi ya siasa ya Kamati kuu ya chama, Kamati ya kudumu ya Ofisi ya siasa ya kamati kuu ya chama, Sekretarieti ya Kamati kuu ya chama, Kamati ya kijeshi ya Kamati kuu ya chama na Kamati kuu ya ukaguzi wa nidhamu. Mkutano wa wajumbe wa nchi nzima wa chama unafanyika mara moja kila mwaka. Wakati mkutano huo unapofungwa, Kamati kuu ya chama ni chombo cha uongozi wa juu kabisa cha Chama cha kikomunisti cha China.

Chama cha kikomunisti cha China hivi sasa kina wanachama karibu milioni 70, katibu mkuu wa chama hicho ni Xi Jinping.

Vyama vya kidemokrasia vya China

Nchini China mbali na Chama cha kikomunnisti cha China, pia kuna vyama vinane vya kisiasa yaani vyama vya kidemokrasia kama vile Kamati ya mapinduzi ya Chama cha Guomintang cha China, Umoja wa demokrasia wa China, Shirikisho la kujenga nchi ya kidemokrasia la China, Shirikisho la kuhimiza demokrasia la China, Chama cha demokrasia cha wakulima na wafanyakazi cha China, Chama cha Zhigong cha China, Shirikisho la elimu la Jiusan na Umoja wa kujiendesha kidemokrasia wa Taiwan. Vyama hivyo vingi vilianzishwa na kuendelea wakati wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan na katika vita vya ukombozi wa nchi nzima. Vyama vya kidemokrasia vinaunga mkono uongozi wa Chama cha kikomunisti cha China, hili ni chaguo lao cha kihistoria katika ushirikiano wa muda mrefu na juhudi za pamoja. Vyama mbalimbali vya kidemokrasia vinafaidika na uhuru wa kisiasa, uhuru wa kujitawala kijumuia na usawa wa hadhi ya kisheria katika eneo lililowekwa kwenye katiba ya nchi. Chama cha kikomunisti cha China na vyama mbalimbali vya kidemokrasia vinafuata sera ya kimsingi ya ushirikiano ya "kuwepo kwa pamoja kwa muda mrefu, kusimamiana, kutendeana kwa moyo safi na udhati, na kushirikiana kwenye dhiki na faraja".

Vyama mbalimbali vya kidemokrasia si vyama visivyo vya tawala, wala vyama vya upinzani, isipokuwa ni vyama vinavyoshiriki mambo ya kisiasa na utoaji wa sera. Hivi sasa wanachama wengi wa vyama mbalimbali vya kidemokrasia wanashika nyadhifa mbalimbali katika Bunge la umma la China na Baraza la mashauriano ya kisiasa kwenye ngazi mbalimbali, vyombo vya serikali na idara za uchumi, utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, kwa mfano wenyekiti wa kamati kuu ya vyama vinane vya kidemokrasia hivi sasa wanashika nyadhifa za manaibu spika wa Bunge la umma la China au manaibu wenyeviti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China. Wakati huo huo, matawi ya vyama mbalimbali vya kidemokrasia pia yanaendelea vizuri katika mikoa na miji mbalimbali nchini China.

Kamati ya Mapinduzi ya Chama cha Guomintang cha China

Kamati ya Mapinduzi ya Chama cha Guomintang cha China kwa ufupi inaitwa Minge, ambacho kilianzishwa tarehe 1 Januari, mwaka 1948, kilianzishwa na kundi la kidemokrasia la Chama cha Guomintang cha China na wazalendo wengine, chama hicho kina umaalum wa shirikisho la kisiasa, ambacho ni chama kinachofanya juhudi katika kujenga ujamaa na kutimiza muungano wa taifa. Chama hicho kina wanachama karibu elfu 65.

Umoja wa demokrasia wa China

Umoja wa demokrasia wa China kwa ufupi unaitwa Minmeng, ambao ulianzishwa mwezi Machi, mwaka 1941, wakati huo umoja huo uliitwa "Shirikisho la vikundi vya kisiasa vya kidemokrasia la China", mwaka 1944 uliundwa upya na kubadilisha jina kuwa Umoja wa demokrasia wa China. Umoja huo ni umoja wa kisiasa wa wasomi wanaoshughulikia mambo ya utamaduni na elimu na wazalendo wanaounga mkono ujamaa, na ni chama chenye malengo ya kijamaa. Idadi ya wanachama wake ni laki 1.56.

Shirikisho la kujenga nchi ya kidemokrasia la China

Kwa ufupi shirikisho hilo linaitwa Minjian, ambalo lilianzishwa mwezi Desemba mwaka 1945, wanachama wake wengi ni wanakampuni na wafanyabiashara wazalendo na wasomi wanaowasiliana nao. Wanachama wake wamefikia elfu 85.

Shirikisho la uhimizaji wa demokrasia la China

Shirikisho hilo linaitwa Minjin kwa ufupi, ambalo lilianzishwa mwezi Desemba mwaka 1945, wanachama wake wengi ni wasomi wa kiwango cha juu na wastani wanaoshughulikia mambo ya elimu, utamaduni, uchapishaji vitabu na sayansi. Shirikisho hilo lina wanachama elfu 81.

Chama cha demokrasia cha wakulima na wafanyakazi cha China

Chama hicho kinaitwa chama cha Nonggong, ambacho kilianzishwa mwezi Agosti mwaka 1930. Chama hicho ni shirikisho la kisiasa la wasomi wa kiwango cha juu na wastani wanaoshughulikia mambo ya afya, sayansi na teknolojia na utamaduni na elimu pamoja na wazalengo wanaounga mkono ujamaa. Idadi ya wanachama wake ni zaidi ya elfu 80.

Chama cha Zhigong cha China

Chama hicho kilianzishwa mwezi Oktoba mwaka 1925, ambacho kiliundwa na wachina waliowahi kuishi ng'ambo na jamaa zao. Idadi ya wanachama wake ni zaidi ya elfu 20.

Shirikisho la elimu la Jiusan

Chama hicho kilianzishwa mwezi Machi mwaka 1946, wanachama wake ni zaidi ya elfu 80 ambao ni wasomi wa kiwango cha juu na wastani wanaoshughulikia mambo ya sayansi na teknolojia, utamaduni na elimu pamoja na afya.

Umoja wa kujiendesha kidemokrasia wa Taiwan

Umoja huo unaitwa Taimeng kwa ufupi, ambao ulianzishwa mwezi Novemba mwaka 1947. Umoja huo ni shirikisho la kisiasa linaloundwa na wazalendo wanaounga mkono ujamaa wa mkoa wa Taiwan wanaoishi China bara.

Vikundi vya Jamii

Shirikisho kuu la wafanyakazi wa China

Shirikisho kuu la wafanyakazi wa China linaitwa Qiuanzong kwa ufupi, ambalo ni chombo cha uongozi cha mashirikisho ya wafanyakazi ya sehemu mbalimbali nchini China, ambalo lilianzishwa tarehe 1 Mei, mwaka 1925.

Jukumu la shirikisho hilo la jamii ni kulinda haki na maslahi halali ya wafanyakazi na haki zao za kidemokrasia; kuwahamasisha na kuwashirikisha wafanyakazi kushiriki katika ujenzi na mageuzi, kukamilisha majukumu ya maendeleo ya uchumi na jamii; kushiriki kwenye usimamizi wa kidemokrasia ya mashirika, na kuwaelimisha wafanyakazi wainue kiwango cha maadili na elimu ya sayansi, tekenolojia na utamaduni.

Shirikisho kuu la wafanyakazi wa taifa la China limeanzisha mawasiliano na uhusiano wa kirafiki na mashirikisho ya wafanyakazi ya kitaifa ya nchi na sehemu zaidi ya 130 duniani. Ilipofika mwishoni mwa mwaka 2002, idadi ya jumla ya wanachama wa shirikisho hilo imefikia milioni 134.

Shirikisho kuu la vijana la taifa la China

Shirikisho hilo lilianzishwa tarehe 4 Mei mwaka 1949 ambalo ni shirikisho la vijana wa makabila mbalimbali wa China.

Jukumu kuu la shirikisho hilo ni kuwakilisha na kulinda haki na maslahi ya vijana wa makabila mbalimbali na sekta mbaimbali za China; kuwaelekeza vijana wafanye juhudi na kushiriki kwenye maisha ya jamii, kufanya juhudi za kuwahudumia vijana kwa ajili ya ukuaji wao mzuri na kuwa watu wenye ujuzi kwa kulitumikia taifa; kuimarisha mawasilliano na mshikamano na vijana wa Taiwan, Hong Kong na Makau pamoja vijana wanaoishi ng'ambo; na kuendeleza mawasiliano na urafiki ma vijana wa nchi mbalimbali duniani.

Kamati ya nchi nzima ya shirikisho kuu la vijana ni chombo chenye madaraka ya juu kabisa, muda wake wa kila awamu ni miaka mitano. Kamati hiyo ina mwenyekiti mmoja na manaibu wenyeviti kadhaa. Wakati wa kufungwa kwa kamati hiyo, halmashauri ya kudumu ya kamati hiyo inaendesha shughuli zake za kila siku.

Shirikisho hilo linatekeleza utaratibu wa wanachama wa makundi, hivi sasa kuna wanachama wa makundi 48, wajumbe 1352

Shirikisho kuu la kina mama wa taifa zima la China

Shirikisho hilo lilianzishwa mwezi Machi mwaka 1949, jina lake la mwanzoni ni Shirikisho kuu la kina mama la kidemokasia la taifa la China, mwaka 1957 jina lake lilibadilishwa kuwa Shirikisho kuu la kina mama la Jamhuri ya Watu wa China, mwaka 1978 jina lake lilibadilishwa kuwa Shirikisho kuu la kina mama la taifa zima la China. Jukumu lake la kimsingi ni: Kuleta mshikamano, kuhamasisha kina mama wengi washiriki katika ujenzi wa uchumi na maendeleo ya jamii, kuwakilisha na kulinda haki na maslahi ya kina mama, na kusukuma mbele usawa kati ya wanaume na wanawake.

Shirikisho kuu la viwanda na biashara la taifa la China

Shirikisho hilo lilianzishwa mwaka 1953, ambalo ni kundi la umma na shirikisho la biashara la kiraia lililoundwa na watu wa sekta za viwanda na biashara wa China.

Jukumu kuu la shirikisho hilo ni kushiriki kwenye mashauriano ya kisiasa, kutoa maoni na mapendekezo na kufanya usimamizi kuhusu sera na hatua kubwa za nchi na masuala makubwa kuhusu siasa, uchumi na maisha ya jamii; kuwaelekeza wanachama wake wafanye juhudi za kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi, kusukuma mbele kazi ya kukamilisha siku hadi siku mfumo wa uchumi wa soko huria wa ujamaa, kusukuma mbele maendeleo ya jamii kwenye sekta zote; kuwakilisha haki na maslahi halali ya wanachama wake, kueleza maoni, matakwa na mapendekezo ya wanachama wake; kutoa huduma mbalimbali kwa wanachama wake; kuanzisha mafunzo ya kazi maalum, kuwasaidia wanachama wake kuboresha usimamizi na uendeshaji wa shughuli, kukamilisha usimamizi wa kazi ya uhasibu, na kuinua teknolojia za uzalishaji na sifa za bidhaa; kuongeza mawasiliano na urafiki na mashirika ya viwanda na biashara na mikoa ya utawala maalum ya Hong Kong na Makau pamoja na sehemu ya Taiwan na ya nchi mbalimbali duniani, na kuhimiza ushirikiano katika sekta za uchumi, teknolojia na biashara.


1  2  3  4  5