18: Mila na Desturi

Mila na Desturi ya Chakula

Desturi ya Kunywa Chai

Wachina wamekuwa na historia ya miaka elfu nne ya kunywa chai. Chai ni kitu ambacho hakiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya Wachina. Wageni wanapofika nyumbani kwa mtu fulani, nao hukaribishwa kwa chai, wanaongea na mwenyeji na huku wanakunywa chai.

Katika Enzi ya Tang kunywa chai kulianza kuwa desturia ya Wachina. Inasemekana kwamba desturi hiyo inahusiana na dini ya Buddha. Mwaka 713 hadi 741, sufii wa dini ya Buddha waliosoma msahafu kwa muda mrefu walikuwa wanajisikia usingizi, basi sufii mzee aliwataka wanywe chai. Tokea hapo njia hiyo ya kuondoa usingizi ilienea kila mahali.

Mwaka 780 mtaalamu wa chai aliandika kitabu cha namna ya kulima, na kutengeneza majani na kunywa chai. Na katika Enzi ya Song mfalme alikuwa anawakaribisha wageni kwa chai.

Nchini China kunywa chai ni aina moja ya utamaduni. Tokea enzi na dahari hadi leo mikahawa ya chai hupatikana kila mahali nchini China, na katika sehemu ya kusini pia kuna vibanda vya chai. Watu wanakunywa chai huku wakiburudika na michezo ya sanaa.

Wachina wa sehemu tofauti pia wana desturi ya kunywa chai tofauti. Watu wa sehemu ya kaskazini wanapenda kunywa chai ya jasmini, watu wa kusini wanapenda kunywa chai ya kijani na baadhi ya watu wanapenda kunywa chai nyekundu.

Namna ya kunywa chai pia ni tofauti kutokana na sehemu tofauti. Watu wa sehemu ya mashariki ya China wanapenda kutumia bilauri kubwa na kutia majani ya chai ndani yake na kisha kumimina ndani ya glasi. Na watu wa sehemu ya kusini wanapenda kumimina maji ya moto ndani ya glasi na kutia majani ndani yake. Adabu ya kunywa chai pia ni inatofautiana kutokana na sehemu tofauti. Mjini Beijing, mwenyeji akileta glasi ya chai, mgeni husimama kuipokea kwa kuonesha heshima na kusema "ahsante". Katika sehemu ya kusini mwenyeji akileta glasi ya chai, mgeni hugongagonga meza mara tatu kwa kidole kuonesha shukrani.

Vijiti vya Kulia

Duniani kuna njia tatu za kupeleka vyakula mdomoni, kwa mkono, kwa kijiko na umma na kwa vijiti vya kulia.

Matumizi ya vijiti vya kulia yalianzia miaka 3000 iliyopita nchini

China. Vijiti vya kulia vinatengenezwa kwa mianzi.

Lakini vipi vijiti vya kulia vilianza kutumika? Inasemekana kwamba watu wa zama za kale walipokula chakula moto moto walikuwa wanatumia vijiti vya mwanzi au vya mti ili kukwepa kuumia vidole. Vijiti vya kulia vina umbo la unene kwa juu na ncha kwa chini na vyenye pembe nne ili kukwepa kuviringika mezani.

Vijiti vya kulia kwa sasa hutengenezwa kwa vitu vya aina mbalimbali, kuna vijiti vya kulia vya shaba, vya pembe za ndovu, na pia kuna vijiti vilivyotiwa fedha kwenye ncha, kama ndani ya chakula kuna sumu fedha hubadilika rangi yake kuwa ya kijani au nyeusi.

Vijiti vya kulia pia ni kama zawadi katika mila ya Wachina. Msichana anayeozwa hupewa jozi mbili za vijiti vya kulia na jozi za mabakuli. Katika sehemu ya kaskazini ya China watu hutupa chumbani kwa maharusi vijiti vya kulia kwa kuashiria watapata mtoto mapema.

Namna ya kutumia vijiti vya kulia ni ufundi mkubwa. Katika nchi za Magharibi kuna klabu ya kufundishia ufundi wa kutumia vijiti vya kulia. Na nchini Ujerumani kuna jumba la kwanza duniani la makumbusho ya vijiti vya kulia, ndani ya jumba hilo kuna vijiti vya kulia vilivyotengenezwa kwa dhahabu, fedha na mifupa ya wanyama. Vijiti hivyo vinatoka nchi tofauti na enzi tofauti.

Mila na Desturi ya Chakula

Wachina husema, ni bora kupata afya kwa chakula kuliko kupata afya kwa dawa. Hii inamaanisha kuwa watu wa China wanatilia maanani sana mchanganyiko wa aina tofauti za vyakula. Ingawa kwa baadhi ya watu wenye hali mbaya kiuchumi ni vigumu kufikia lengo hilo, lakini watu wenye uchumi mzuri hutilia maanani sana mchanganyiko wa aina tofauti za vyakula. Miaka nenda miaka rudi vyakula maalumu vimetokea katika siku maalumu, kwa mfano, vyakula vya maingiliano ya kijamii, vyakula vya ndoa na vya maombolezo, vyakula vya sikukuu ya kuzaliwa kwa wazee na vyakula vya siku za uzazi.

Vyakula vya mawasiliano ya kijamii inamaanisha vyakula vilivyoandaliwa kwa ajili ya kuwakaribisha marafiki, jamaa, kusherehekea kupata mtoto, au kuhamia nyumba mpya.

Watu wa sehemu tofauti pia wana desturi tofauti ya kuwakaribisha wageni. Katika sehemu ya kaskazini wenyeji huwakaribisha wageni kwa tambi, na kama wageni wanashinda nyumbani huwa wanakaribishwa kwa Jiaozi katika siku ya pili. Katika sehemu ya kusini, wageni wanapofika tu wenyeji huwamiminia chai na mara wanaingia jikoni kuwapikia keki au kuchemsha mayai yaliyotiwa sukari, na baadaye hupika chakula hasa.

Katika mji wa Quanzhou wageni hukaribishwa kwa matunda.

Katika mji wa Beijing wenyeji huwakaribisha wageni kwa vitoweo vya aina nane, na katika sehemu ya kaskazini ya China wenyeji huwakaribisha wageni kwa vitoweo viwili viwili sawa. Vyakula kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa wazee, vyakula huwa ni tambi pamoja na vitoweo, ikimaanisha maisha marefu.

Vyakula vya Dawa

Katika China ya kale watu walipata dawa kutoka kwenye mimea na kupata dawa za mitishamba. Mazao ni chakula na baadhi pia ni dawa. Wachina wanasema, "ni bora kupata afya kwa chakula kuliko kwa dawa, na kinga ni bora kuliko tiba."

Chakula ambacho pia ni dawa ni mila ya upishi wa tiba. Katika Enzi ya Zhou (1046 K.K.—256 K.K.) chakula hicho kilianza kutumika katika tiba. Katika Enzi ya Tang (618—907) mtaalamu wa tiba Sun Simao alieleza mengi kuhusu kutibu magonjwa kwa chakula katika kitabu chake ambacho kimekuwa na athari kubwa kwenye tiba ya Kichina hadi leo.

Bw. Sun Simao aliona kuwa afya inapatikana kwa chakula kinachofaa. Mtu akiwa mgonjwa, kwanza atibiwe kwa chakula, kama hakisaidii kitu basi baadaye atumie dawa.

Sun Simao aliishi kwa zaidi ya miaka 100, maisha yake marefu yanawafanya watu waamini kuwa chakula chenye uwezo wa kutibu ugonjwa ni msingi wa kupata afya bora.

Chakula cha dawa kinatumika sana katika matibabu ya magonjwa, na baadhi ya vyakula vinavyotibu magonjwa fulani vinajulikana miongoni mwa wenyeji. Kwa mfano, mtu akipata mafua, anatakiwa anywe maji moto moto yaliyochemshwa kwa tangawizi, vitunguu vya majani na sukari guru, atatokwa jasho na kupona.

Katika chakula cha dawa pia kuna maua. Kupika aina fulani ya maua kama vitoweo kuliwahi kutumika sana katika Enzi ya Tang.

Nchini China kuna aina za maua kiasi cha elfu moja, na aina mia moja hivi zinaweza kutumika kama ni chakula cha dawa, na katika sehemu ya kusini ya China aina hizo zinafikia zaidi ya 260.

Maua yanayotumika kama chakula yanawasaidia zaidi wanawake. Kwa mfano maua ya waridi, yanasaidia sana kwa kurekebisha hedhi na rangi ya ngozi.

Chakula chenye uwezo wa dawa hupikwa kwa uji, na vitoweo. Kuna mikahawa ya chakula cha dawa ambayo hupikwa kwa ajili ya kusaidia tiba ya ugonjwa fulani.

Sheria ya chakula nchini China inasema, ni marufuku kutia dawa ndani ya chakula. Kwa ajili ya chakula chenye uwezo wa kutibu magonjwa kisikiuke sheria hiyo, idara ya afya imeruhusu mitishamba kumi kadhaa kutiwa kwenye chakula, kama vile tende, tangawizi, nanaa n.k.

Chakula chenye uwezo wa kutibu magonjwa kimeenea sana nchini China na pia duniani. Pombe na chai yenye maua au magamba ya matunda fulani na mizizi ya mimea fulani vimekuwa vinywaji vya kila siku katika nchi za nje.

Vyakula vya Aina Tatu katika Sikukuu Tatu

Nchini China kuna sikukuu tatu kubwa, nazo ni sikukuu ya taa, sikukuu ya mashindano ya mbio za mashua ya dragoni na sikukuu ya mwezi kwa kalenda ya Kichina. Katika sikukuu hizo tatu kuna vyakula maalumu.

Tahere 15 ya mwezi wa Januari kwa kalenda ya Kichina ni sikukuu ya taa. Katika siku hiyo watu wa China wana mila ya kula vidonge vitamu vya unga unaonata, Wachina wa sehemu ya kaskazini wanaviita vidonge hivyo kwa jina la Yuanxiao , na watu wa sehemu ya kusini wanaita kwa jina la Tangyuan , na namna za kutengeneza zinatofautiana.

Katika sehemu ya kaskazini ya China vidonge hivyo hutengenezwa kwa unga wa mchele unaonata, na ndani ya vidonge hutiwa vijazo vya sukari, simsim, karanga iliyosagwa. Kila sikukuu hiyo inapokaribia vidonge hutayarishwa madukani,

Katika sehemu ya kusini ya China watu hutengeneza vidonge vidogo vidogo na kutia vijazo vyenye chembe za karanga, simsim, unga wa tende na kunde nyekundu.

Vidonge hivyo huchemshwa, ni laini na ni vitamu, ikimaanisha kuungana kwa jamaa.

Sikukuu ya mashindano ya mbio za mashua ya dragoni iko katika tarehe tano mwezi wa tano kwa kalenda ya Kichina. Katika siku hiyo Wachina wana mila ya kula Zongzi , chakula ambacho mchele unaonata pamoja na tende hufungwa kwa majani ya matete kama sambusa na kuchemshwa. Vijazo ndani ya Zongzi huwa tofauti kati ya sehemu ya kaskazini na kusini.

Masimulizi ya mapokeo yanasema kuwa watu wana mila ya kula Zongzi ili kumkumbuka mshairi mkubwa Qu Yuan. Karne ya tatu dola la Chu aliloishi Qu Yuan lilitekwa, kutokana na huzuni na hasira Qu Yuan alijitupa ndani ya mto tarehe 5 mwezi wa tano kwa kalenda ya Kichina. Watu wa wanaofuata walianza kutengeneza Zongzi na kutupa mtoni kumfanyia tambiko.

Zongzi ni chakula na pia ni zawadi kwa marafiki na jamaa. Katika siku hiyo marafiki na jamaa hutembeleana na kupeana Zongzi .

Tarehe 15 Agosti kwa kalenda ya Kichina ni sikukuu ya mwezi, kwa sababu katika siku hiyo mwezi ni mviringo na unang'ara kabisa katika mwaka mzima. Watu huburudika kwa mwezi wakati usiku na huku wakila keki za duara mithili ya mwezi. Ndani ya keki hutiwa vijazo vya aina tofauti.

Keki hutengenezwa kwa duara mithili ya mwezi mviringo. Katika siku za kale watu walikuwa wanaandalia keki hizo uani na kuabudu mwezi. Baada ya ibada wanakula keki hizo. na siku hiyo pia ina maana ya kujumuika kwa jamaa wanaoishi katika sehemu tofauti, wanakula pamoja katika usiku huo wenye mwezi mpevu.

Keki za mwezi hupikwa kwa ladha tofauti kutokana na sehemu tofautu nchini China.

Kufuatana na jinsi maisha yanavyokuwa bora keki hupikwa kwa vijazo vilivyo bora zaidi, kuna vijazo vya sukari, unga wa tende, unga wa kunde nyekundu, nyama, kiini cha yai la bata, vipande vya matunda na krimu.

Keki za mwezi pia ni zawadi kwa jamaa na marafiki. Katika siku za kabla ya sikukuu hiyo keki za mwezi hujaa madukani.

Jiaozi (sambusa ndogo za Kichina)

Jiaozi ni aina moja ya utamaduni wa Kichina, kwa kuwa chakula cha jadi cha Kichina kinaonesha ukarimu na furaha kubwa kwa kujiwa na wageni. Kama mgeni fulani kutoka ng'ambo hajawahi kula Jiaozi wengine husema alifika China bure.

Kwa kifupi Jiaozi ni kijazo kilichofungwa kwa unga wa ngano. Katika siku za zamani, Jiaozi ilikuwa inapikwa katika sikukuu tu hasa katika usiku wa kuamkia sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina.

Kijazo cha Jiaozi kina aina tofauti ya mboga na ya nyama au mchanganyiko wa mboga na nyama. Watu hutayarisha kijazo kwa kukatakata nyama mpaka kima na kukatakata mboga mpaka chembe, na kisha hutia soyasosi, mafuta ya simsim, na viungo vingine, vishindo vya kukatakata nyama na mboga vinaashiria maisha mazuri.

Baada ya vijazo kuwa tayari, hufungwa kwa unga kama sambusa ndogo na kuweka mezani tayari kwa kuchemsha.

Baada ya kutia Jiaozi ndani ya maji yaliyochemka, Jiaozi huzama chini na baada ya muda huelea juu, katika muda wa kuchemsha kuna haja ya kutia maji kidogo baridi mara tatu kila baada ya dakika chache, kiasi cha dakika ishirini hivi huiva.

Wakati wa kula Jiaozi pia kuna adabu maalumu, bakuli la kwanza ni kwa ajili ya wahenga na wazee marehemu, bakuli la pili ni kwa ajili ya mungu wa jiko, na kuanzia bakuli la tatu watu wanaanza kula, lakini kwanza kwa wazee.

Katika mkesha wa mwaka mpya wa Kichina, Jiaozi ni chakula cha lazima, jamaa wa familia moja hata akiwa mbali na nyumbani lazima arudi na kujumuika na jamaa zake kula Jiaozi pamoja.

Katika siku hizi, kutokana na shughuli nyingi za kazi, watu hupata Jiaozi iliyoganda kwa baaridi na katika maduka ya kujihudumia na kuchemsha nyumbani au jamaa wote wanakula katika mikahawa, na adabu nyingi za zamani zimekuwa hazifuatwi sana hata vijijini.


1 2 3 4