19: Opera

Hadithi kuhusu michezo ya sanaa

Mtoto Yatima Zhao

Karne ya 8 hadi 5 K.K. kilikuwa ni kipindi cha Spring na Autumn, kulikuwa na madola mengi, na kati ya madola hayo kulikuwa na Dola la Jin. Katika dola hilo walikuwepo maofisa wawili wakubwa, mmoja ni wa ukatibu aliyekuwa mwaminifu kwa mfalme, aliitwa Zhao Dun, na mwingine ni ofisa wa jeshi aliyeitwa Tu Angu. Watu hao wawili walikuwa hawaelewani. Tu Angu alitaka kumwua Zhao Dun kwa hila.

Tu Angu alichemsha ubongo namna ya kumwua Zhao Dun kwa hila. Mfalme wa Dola la Jin kweli alidanganywa akiamini kuwa Zhao Dun ni msaliti wa taifa, aliamuru kumwua na watu wote wa familia yake isipokuwa mkamwana wake Zhuang Ji, kwa kuwa yeye ni binti wa mfalme lakini alifungiwa kwenye kasri.

Wakti huo Zhuang Ji alikuwa mja mzito na muda mfupi baadaye alizaa mtoto mmoja wa kiume, aliitwa "Mtoto Yatima Zhao", mama yake alitumai kuwa mtoto huyo atalipiza kisasi kwa ajili ya familia ya Zhao. Ofisa Tu Angu alipata habari kuwa binti wa mfalme alizaa mtoto, alituma watu kulinda mlango wa kasri na kumwua mtoto huyo alipotimiza mwezi mmoja ili kufyeka mzizi utakaohatarisha usalama wake baadaye. Zhao Dun alikuwa na rafiki mmoja mkubwa kwa jina la Cheng Ying, alikuwa ni daktari. Ili kumwokoa mtoto huyo yatima, alibeba sanduku lake la dawa alijidai kwenda kumtibu binti wa mfalme. Alitia mtoto ndani ya sanduku lake na kutaka kumtorosha nje ya kasri. Lakini alipofika kwenye mlango wa kasri aligunduliwa na jemadari Han Jue aliyelinda mlango. Han Jue pia alimhurumia sana mtoto huyo alimwachia huru, lakini yeye mwenyewe alijiua kwa kisu.

Tu Angu alipofahamu kuwa mtoto ametoroshwa, akaamuru kwamba kama katika muda wa siku tatu mtoto huyo hajagunduliwa atawaua watoto wote nchini walio chini ya umri wa mwaka moja.

Cheng Ying alishauriana na rafiki mwingine wa Zhao Dun aliyeitwa Gong Sunchujiu, waliona kuwa njia moja tu ya kuweza kuwaokoa watoto wote wa dola la Jin, nayo ni kumwacha mtoto mmoja mwingine auawe badala ya mtoto yatima. Cheng Ying alikuwa na mtoto mmoja ambaye alilingana na mtoto yatima kwa umri. Basi Cheng Ying kwa uchungu alimpa Gong Sunchujiu mtoto wake na alikwenda kupiga ripoti kwa kusema kuwa Gong Sunchujiu alimficha mtoto yatima. Basi Gong Sunchujiu na mtoto wote waliuawa.

Miaka 15 baadaye, jemadari mwaminifu Wei Jiang alikuja kutoka mpakani, aliposikia kwamba watu wa familia Zhao Dun wote waliuawa na Cheng Ying alipiga ripoti alikasirika sana hata alimchapa viboko vikali Cheng Ying.

Cheng Ying alikuwa kimya alipochapwa viboko, akifikiri kuwa viboko vikali vinaonesha chuki zake kwa msaliti, na atasaidia mtoto yatima kulipa kisasi. Baada ya kubaini uaminifu wa Wei Jiang alimwambia yote jinsi alimtoa mtoto wake na Gong Sunchujiu alivyouawa kwa ajili ya kumwokoa mtoto yatima. Wei Jiang alisisimka na kumwahidi atamsaidia mtoto yatima kulipiza kisasi.

Baada ya kurudi nyumbani Cheng Ying alimwambia yote ya zamani kwa picha. Mtoto yatima alielewa kisa chake akadhamiria kulipiza kisasi.

Mkoba wa vito "Suolinnang"

Katika zama za kale alikuwepo mfanyabiashara mmoja tajiri katika sehemu ya Dengzhou, tajiri huyo alikuwa na binti moja aliyeitwa Xiang Ling, watu wa familia wote walimpenda sana. Xiang Ling alifikia umri wa kuolewa, wazazi wake walimtayarishia zawadi nyingi za ndoa, na mama yake alimshonea mkoba mmoja uliotariziwa, na ndani yake vilitiwa vito vya kila aina. Inasemekana kuwa msichana akiwa na mkoba kama huo atapata mtoto mwerevu wa kiume.

Katika siku ya ndoa, Xiang Ling alikaa ndani ya kibanda cha bibi harusi cha kubebwa, watu waliomsindikiza walimpigia vigelegele. Njiani mvua kubwa ilinyesha, walikimbia kwenye kibanda kimoja, lakini punde kidogo alikuja bibi harusi mwingine aliyekaa ndani ya kibanda cha harusi, lakini kibanda chenyewe kilikuwa kidogo na kichakaa. Bibi harusi ndani ya kibanda hicho alilia kwa kwikwi. Xiang Lian aliposikia kilio aliwatuma kijakazi na mtumishi mmoja mzee waende kuangalia kulikoni. Bibi harusi huyo aliitwa Zhao Shouzhen, familia yake ilikuwa maskini sana, na mama yake alikufa mapema, aliyebaki ni baba yake tu ambaye alikuwa hana zawadi ya ndoa. Zhao Shouzhen alihofia atachekwa na wengine kutokana na umaskini na kuwa na wasiwasi kwamba hakuna mtu wa kumtunza baba yake, kwa hiyo alilia machozi.

Kusikia habari hiyo, Xiang Ling alimhurumia sana, akakumbuka jinsi alivyokua katika familia yenye hali nzuri na hakujua kwamba duniani kuna watu maskini kama Zhao Shaozhen. Xiang Ling alifikiri atawezaje kumsaidia? Ghafla aligundua mkoba wake, basi alimpa Zhao Shouzhen bila kutaja jina lake. Wakati huo mvua ilisimama, vibanda viwili vya bibi harusi viliendelea kubebwa na kila kimoja kushika njia yake.

Baada ya miaka sita kupita, katika sehemu ya Dengzhou yalitokea mafuriko, Xiang Ling na mumewe na mtoto walipoteana. Xiang Ling peke yake alizurura zurura hadi sehemu ya Caizhou, maisha yalikuwa magumu sana. Lakini kwa bahati huko alimkuta yaya wake wa zamani ambaye alimwongoza hadi kwenye familia tajiri ya Lu kuwa yaya kumtunza mtoto aitwaye Tian Lin. Tian Lin alikuwa na umri wa miaka mitano tu, alimpenda sana Xiang Lin na kila siku alimtaka acheze naye mpira bustanini.

Siku moja mtoto Tian Lin alirusha mpira ndani ya jumba dogo la ghorofa. Xiang Ling aliingia ndani kutafuta mpira, ghafla aligundua mkoba mmoja ukutani, alichunguza kwa makini mkoba huo ndio aliyompa Zhao Shouzhen. Mbele ya mkoba huo alikumbuka jinsi alivyotengana na mume na mtoto wake, alilia. Mtoto Tian Lin alipoona alilia, alikimbilia kumwambia mama yake. Mama wa Tian Lin ndiye Zhao Shaouzhen, aliolewa na Bw. Lu, na kutokana na mkoba wa vito familia yake ilikuwa imetajirika siku hadi siku. Zhao Shouzhen hakumsahau mfadhili wake, akajenga jumba dogo la ghorofa na kutundika mkoba huo ukutani ikionesha hatamsahau daima. Aliposikia yaya akilia alipoona mkoba, alikwenda kumwuliza aliolewa lini na hali ya njiani ilikuwaje. Xiang Lin alimweleza hali ilivyokuwa, akafahamu kuwa Xiang Ling ndiye mfadhili wake, alifurahi sana na kwa haraka alimletea nguo za gharama na kumtendea kama mgeni wa kuheshimiwa sana, na alimsaidia kuwatafuta jamaa zake.

Muda mufupi baadaye, mume wa Xiang Ling akiwa na mtoto wake pia walikuja katika sehemu ya Caizhou, alisikia kwamba mkewe alikuwa yaya katika familia ya Lu, alikwenda kwa familia hiyo, jamaa wa familia hiyo walikutana. Xiang Ling na Zhao Zhouzhen walikuwa marafiki wakubwa.

Si Lang Aenda Kumtazama Mama Yake

Katika karne ya 10 hadi 12 nchini China kulikuwa na madola mawili, moja ni Dola la Liao kaskazini mashariki mwa China, moja ni Enzi ya Song, katikati ya China. Mara kwa mara madola hayo mawili yalikuwa yanapigana.

Katika Enzi ya Song kulikuwa na ukoo mmoja wa majemadari uliitwa ukoo wa Yang, baba aliitwa Yang Linggong, mama aliitwa She Taijun, walikuwa na watoto wa kiume wanane ambao wote walikuwa hodari wa kupigana vita na walitoa mchango mkubwa kwa ajili ya ulinzi wa taifa.

Mfalme wa Dola la Liao alipanga njama, akimwalika mfalme wa Enzi ya Song kwenda kufanya mazungumzo ya amani. Kutokana na kutofahamu ukweli ulivyo, ili kumlinda mfalme, mtoto wa kwanza wa ukoo wa Yang alijipamba kuwa mfalme alikwenda Dola la Liao kwa kulindwa na ndugu zake saba. Njiani walishambuliwa na askari wa Dola la Liao kwa kuviziwa, ndugu watatu waliuawa, na mtoto wa nne aliyeitwa Si Lang alitekwa nyara. Kutokana na kuwa Si Lang alitumia jina jingine Mu Yi badala la ya jina lake halisi, alifanikiwa kuwadanganya askari wa Dola la Liao.

Mama mfalme Xiao wa Dola la Liao aliona kuwa Mu Yi ana sura nzuri na ni hodari wa vita, alimwoza binti yake Tie Jing kwake, hivyo Si Lang aliyetumia jina la Mu Yi alikuwa mume wa binti wa mfalme. Waliishi vizuri na baadaye walipata mtoto mmoja wa kiume, lakini wote walikuwa hawajui kama mume wa binti wa mfalme alikuwa mtoto wa nne wa ukoo wa Yang.

Madola mawili yaliendelea kupigana. Baada ya miaka 15 Dola la Liao kwa mara nyingine tena lilishambulia Enzi ya Song. Si Lang na binti wa mfalme na mama mfalme wote walikwenda kwenye medani ya vita. Mfalme wa Enzi ya Song alimtuma mtoto wa sita wa Ukoo wa Yang kuwa jemadari kwenda kwenye medani, na mama yake She Taijun pia alifuatana naye kuwahudumia askari na farasi kwa chakula.

Si Lang alipofahamu kwamba mama yake na ndugu yake walikuja kwenye medani ya vita aliwawazia sana akitaka kwenda kuonana nao. Lakini kutokana na sheria ya kijeshi, bila ya kibao cha ruhusa ya mfalme asingeweza kutoka kituo cha ukaguzi. Si Lang alikuwa na wasiwasi mkubwa, lakini hakuweza kumwambia mwingine ukweli wa mambo. Binti wa mfalme alipoona kila wakati mumewe alikuwa kimya na kuonekana kuwa na jakamoyo, alimdadisi. Mwishowe Si Lang alimwambia ukweli wenyewe, kwamba jina lake la ukoo ni Yang, ni jemadari wa Enzi ya Song, alitaka sana kuonana na mama yake. Si Lang alimsihi sana mkewe amsaidie kupata kibao cha ruhusa ya mfalme. Binti wa mfalme mwenye roho nzuri alimwahidi atakwenda kwa mama yake kuiba kibao hicho, lakini huku alikuwa na shaka kuwa Si Lang akienda hatarudi tena, wakati huo Si Lang aliapa atarudi usiku katika siku atakapoondoka.

Bindi wa mfalme alimchukua mtoto wake kwenda kwa mama yake, alipokuwa kwa mama yake alimfinya mtoto wake na mtoto mara alilia kwa kelele. Mama mfalme alimpenda sana mjukuu wake, mara akampakata na kumbembeleza. Binti wa mfalme alimwambia mama yake kuwa mtoto anataka kucheza na kibao cha ruhusa. Kwa kumpenda sana mjukuu wake alimpa kibao hicho na kumwambia binti yake kuwa siku ya pili akirudishe.

Si Lang akiwa na kibao cha ruhusa alipita kituo cha ukaguzi akafika kwenye kambi ya jeshi la Enzi ya Song, alionana na ndugu yake na walizungumzia hali ya vita vilivyoshindwa miaka 15 iliyopita na kusababisha kutengana kwao, ndugu wawili walikumbatiana huku wakilia. Baadaye Si Lang alikwenda kwa mama yake She Taijun. Mama mzee mwenye mvi alipoona mwana wake Si Lang asiyekuwa na habari kwa miaka mingi aliona mshtuko na furaha, mama na mwana walielezana jinsi walivyokumbukana sana. Wakati ulipita haraka, kukapambazuka, Si Lang aliagana na mama yake kwa moyo wa upendo na kurudi kambi yake.

Si Lang alipopita kituo cha ukaguzi aligunduliwa kuwa ni mume wa binti wa mfalme, mara alipelekwa mbele ya mama mfalme. Mama mfalme hakutegemea kuwa mkwe aliyemchagua ni jemadari wa Enzi ya Song, na zaidi ya hayo binti yake alimsaidia kwenda kwenye kambi ya adui kumwona mama yake, alikasirika sana, mara alitaka kumwua. Binti mfalme kwa haraka alimchukua mtoto wake kwenda kumbembeleza mama mfalme mpaka amsamehe Si Lang, na kumruhusu aweze kurudi nyumbani kumtazama mama yake.

Kibanda cha Maua ya Peony

Katika enzi za kale, alikuwepo mkuu mmoja wa wilaya aliyeitwa Du Bao. Mkuu huyo alikuwa na binti mmoja aliyeitwa Du Liniang, alikuwa mrembo na mwerevu. Baba yeke Du Bao alimpatia binti yake mwalimu wa kumfundisha kila siku nyumbani, na kijakazi aliyeitwa Chun Xiang pia alisoma pamoja naye, lakini kijakazi huyo alikuwa na tabia ya utukutu, mara kwa mara alikuwa anatoka nje kucheza cheza.

Katika jamii ya kimwinyi nchini China, ndoa ilikuwa inapangwa na wazazi, msichana alikuwa anaolewa na mume ambaye hata hakuwahi kumwona. Kutokana na kusoma vitabu vya kale, Du Liniang alipenda sana ndoa yake iwe kujichagulia mwenyewe.

Majira ya Spring yalifika, Chun Xiang alimwambia Du Liniang kuwa nyuma ya nyumba kuna bustani nzuri. Kwa kuwa na Du Liniang alikuwa anafuata maadili ya umwinyi, kila siku ya mwaka mzima alikuwa anajifungia chumbani kusoma na kutaziri tu. Kutokana na kushawishiwa na Chun Xiang, kisirisiri alikwenda kwenye bustani. Mandhari ya bustani ilikuwa nzuri kweli, maua ya aina mbalimbali yalikuwa yamechanua, miti mikubwa mikubwa na ndege wa kila aina walikuwa wanalia lia na kuruka ruka. Mbele ya mandhari hiyo nzuri, Du Liniang alifikiri, kila siku alijifungia tu ndani ya nyumba, ujana wake utakuwa kama mandhari ya bustani hiyo kwamba itapotea baada ya majira, maua yatasinyaa, majani yatapukutika. Kama uzuri haukumfurahisha mtu yeyote, basi uzuri huo hauna maana yoyote. Du Liniang akiwa na wazo hilo alirudi chumbani kwake, na kutokana na uchovu mara alipata usingizi wa mang'amung'amu.

Katika ndoto yake, alirudi tena kwenye bustani, alikutana na kijana mmoja msomi mwenye kitabu mkononi, waliongea naye. Kijana huyo alimpenda Du Liniang kwa uzuri wake na werevu wake na kumsikitikia kupoteza ujana bure. Du Liniang aliona kijana huyo kweli anamfahamu sana, alianza kumpenda moyoni mwake.

Mama yake alipokuja chumbani alimzindua Du Liniang kutoka kwenye ndoto nzuri. Baadaye alikwenda tena kwenye bustani na kutafuta ndoto yake. Mandhari ilikuwa ni ile ile, lakini kulikuwa hakuna kijana msomi. Alimtafuta tafuta na huku akimkumbuka kumbuka, asimpate. Alihuzunika sana na baada ya kurudi chumbani akawa mgonjwa. Kila siku alikuwa anakumbuka ile ndoto nzuri, alijichorea picha yake na kumwomba Chun Xiang aiweke katika bustani kwenye mlima wa bandia, muda si muda alifariki. Kabla ya kufa, aliwaomba wazazi wake wamzike katika bustani kwenye mti mmoja mkubwa, na kumwekea jiwe la kaburi.

Baadaye, wazazi wa Du Liniang walihama. Baada ya siku chache kijana mmoja msomi alipita kwenye bustani hiyo, na bahati mbaya aliugua, akapumzika karibu na bustani. Kijana huyo aliitwa Liu Mengmei, ambaye ndiye Du Liniang aliyemkuta ndotoni.

Baada ya kupona, kijana Liu Mengmei alitembelea bustani, kwa bahati aliona picha ya Du Liniang, aliona sura ya picha hiyo si ngeni kwake, akaichukua picha hiyo na kubandika ukutani. Kila siku aliiangalia na kila alipoigangalia alizidi kupenda, na aliichukulia picha kama ni mtu hai.

Du Liniang ingawa alikufa lakini alibakiza muzimu wake kwenye bustani. Alipoona kijana huyo kweli anampenda sana, basi alikuja chumbani na kukaa na kijana kila siku, na kuondoka asubuhi. Kijana Liu Mengmei alimwuliza atawezaje kuishi naye siku zote. Du Liniang alisema: Pindi akifukua kaburi lake, atafufuka. Kijana huyo alifurahi sana, na mara akaenda kwenye kaburi, akafukua kaburi na Du Liniang kweli alifufuka, alikuwa mrembo kama zamani. Tokea hapo walikuwa mume na mke na kuishi kwa furaha kila siku.

Hadithi ya msichana Du Liniang aliyekufa kwa ajili ya mapenzi na kufufuka kwa ajili ya mapenzi vile vile inawasisimua watu wengi.

Hadithi ya Joka Jeupe

Katika enzi za kale, kwenye Mlima wa Emi kulikuwa na majoka mawili yenye umri wa miaka elfu moja, moja jeupe, moja jeusi. Majoka hayo mawili yalipenda sana mandhari ya watu wanapoishi, basi yalijibadilisha kuwa wasichana wawili warembo, moja lilijipa jina la Bai Suzhen , jingine liliitwa Xiao Qing. Siku moja walifika kwenye sehemu maarufu yenye mandhari nzuri, ziwa la Xihu mjini Hangzhou.

Mandhari ya ziwa la Xihu kweli ilivutia sana, walipofika kwenye daraja moja la ziwa hilo ghafla mvua ilianza kunyesha, wakakimbia mvua na kujificha chini ya mti mmoja mkubwa. Wakati huo alikuja kijana mmoja mwenye mwamvuli aliyeitwa Xuxian, ambaye alikuwa akirudi nyumbani baada ya kusafisha makaburi. Alipoona wasichana chini ya mti aliwasaidia kwa mwamvuli wake na baadaye aliwasaidia kuwapeleka nyumbani kwa mashua. Bai Suzhen alianza kumpenda kijana huyo, alipoagana na kijana huyo alimwambia kesho aje kuchukua mwamvuli wake. Siku ya pili kijana Xuxian alifika nyumbani kwa Bai Suzhen karibu na ziwa kuchukua mwamvuli wake. Bai Suzhen alimshukuru sana na kumwuliza habari za familia yake, akafahamu kuwa alifiwa na wazazi wake mapema tokea alipokuwa mtoto na sasa anaishi kwa dada yake na kufanya kazi katika duka moja la dawa. Msichana Bai Suzhen aliomwomba aolewe naye. Hakika Xu Xian alikuwa na furaha isiyo kifani. Kwa kuongozwa na Xiao Qing walifanya sherehe ya ndoa. Baada ya ndoa walianzisha duka la dawa. Bai Suzhen alifahamu matibabu, kila siku aliwatibu wagonjwa wengi.

Kulikuwa na sufii mmoja wa dini ya Buddha aliyekuwa anaitwa Fa Hai. Fa Hai alikuwa anajua siri ya Bai Suzhen kuwa alikuwa joka mwenye miaka elfu moja, na hakika angewadhuru watu, hivyo alidhamiria kumwokoa kijana Xu Xian.

Siku moja Fa Hai alikuja nyumbani kwa Xu Xian, alimwambia, mkewe ni zimwi. Xu Xian hakuamini. Basi Fa Hai alimwambia, kama haamini, ajaribu kumshawishi anywe pombe tarehe 5 Mei, siku ya mashindano ya mbio za mashua, na kama akinywa atarudia asili yake.

Tarehe 5 Mei ilifika, kila familia hunywa pombe kusherehekea siku hiyo. Majoka yanaogopa pombe, Bai Suzhen alitaka kwenda mlimani kukwepa, lakini alikuwa na wasiwasi kuwa mumewe Xu Xian atamshuku, alikuwa hana budi ila kubaki nyumbani akijidai anaumwa.

Ingawa Xu Xian hakuamini aliyoambiwa na sufii Fa Hai, lakini kila mmoja katika siku hiyo hunywa pombe, hivyo alimshawishi mkewe anywe pia. Mkewe Bai Suzhen alishindwa kukataa, alikunywa glasi moja, mara akaanza kuona kizunguzungu. Xu Xian alimsaidia hadi kitandani, kisha akaenda jikoni kumtengenezea supu ya kuondoa ulevi. Akaja na bakuli moja la supu kitandani, alipofungua chandarua akaona joka kubwa jeupe limelala kitandani, Xu Xian alikufa kwa mshtuko.

Joka jeupe lilipozinduka likaona mumewe amekufa kwa mshtuko, alihuzunika sana, alimwomba Xiao Qing amtunze mumewe, na yeye akatoka haraka na kwenda kwenye mlima mmoja ulioitwa Xianshan ambako kulikuwa na aina moja ya jani la dawa ambalo lingeweza kumwokoa mumewe.

Wakati huo Bai Suzhen alikuwa amepata mimba ya miezi saba. Alipofika mlima Xianshan watoto waliokuwa wananlinda mlima walipojua kuwa anataka kuiba jani la ajabu walipambana naye. Mungu wa mlima huo alipoona jinsi Bai Suzhen alivyohangaika kumwokoa mumewe alimpa jani la ajabu.

Xu Xian alifufuka, lakini bado alikuwa ameshikwa na hofu. Bai Suzhen alipatia mzungu wa kumdanganya, alitumia kitambaa kirefu cheupe na kukigeuza kuwa joka kuzunguka kwenye boriti la dari na kumwita mumewe aone. Kwa kuona joka hilo, Xu Xian aliondoa mashaka yake juu ya mkewe, na waliendelea kuishi kwa mapenzi.

Sufii Fa Hai hakukufa moyo. Siku moja alimdanganya Xu Xian kwenda kwenye hekalu lake na kumzuia asirudi nyumbani. Baadaye mkewe na Xiao Qing walikuwa kwenye hekalu wakitaka kumrudisha nyumbani, wakagombana na sufii. Wakati walipopurukushana, Bai Suzhen alisikia maumivu ya uja uzito, kwa haraka alirudi nyumbani na Xiao Qing, alipofika kwenye daraja alikumbuka jinsi alipokutana na mumewe na kuanza na mapenzi, alihuzunika sana. Xiao Qing alimlaumu Xu Xian kwa kumsikiliza sufii, alimshawishi Bai Suzhen amwache mumewe.

Kwa kusaidiwa na sufii wengine, Xu Xian alitoroka kutoka hekalu na kwenye daraja alimpata mkewe. Mkewe alimwambia ukweli wa mambo, kwamba kweli alikuwa joka. Wakati huo Xu Xian alikuwa ameelewa kwamba mapenzi ya mkewe ni ya kweli na makubwa, akamwahidi kuwa hatajali akiwa ni kitu gani, lakini ataishi naye mpaka kufa.

Baada ya kurudi nyumbani, muda mchache baadaye Bai Suzhen alizaa mtoto. Katika siku ya kutimiza mwezi mzima kwa mtoto walifurahi sana, lakini wakati huo sufii Fa Hai alikuja tena nyumbani, alimkamata Bai Suzhen na kumtia chini ya mnara wa Leifong kando ya ziwa la Xihu.

Xiao Qing alitorokea mlimani Emei, alijitahidi kuinua uhodari wake wa mapambano, mwishowe alimshinda Fa Hai, na alimwokoa Bai Suzhen.

Mapenzi ya Dhiki

Mke wa Zhong Shanwang aliyeitwa Liang Qi kwa kuogopa kupoteza mapenzi ya mumewe kwa kutokuwa na mtoto wa kiume, alibadilishana mtoto wake wa kike aliyezaliwa siku chache kwa mtoto wa kiume na kuchapa alama nyekundu kwenye bega la mtoto wake halisi wa kike. Mtoto aliyepata alimpatia jina la Xu Tian Bao.

Baada ya miaka 18 mhuni mmoja aliyeitwa Chang Ming siku moja alivamina na kumpora mwimbaji mwanamke Li Ying na alimwua baba yake, lakini baadaye Xu Tianbao alimwokoa mwimbaji huyo Li Ying. Kutokana na kuhofu kuwa mhuni Chang Ming atalipiza kisasi, alimficha nyumbani kwa mtu, siku nenda siku rudi walikuwa na mapenzi, na waliahidiana kufunga ndoa baadaye. Lakini mama wa Tian Bao alimdharau Li Ying aliyetoka ukoo maskini, alikwenda kwa mwimbaji huyo na kumpiga, ghafla aligundua alama nyekundu begani. Wakati huo mfalme alimchagua Tian Bao kuwa mume wa binti yake. Tian Bao alikuwa hana njia ila kukubali lakini moyoni aliendelea kumpenda Li Ying na kumpuuza binti wa mfalme. Binti wa mfalme alikasirika, alitaka kumwua Li Ying, Tian Bao alimpiga katika ugomvi.

Binti wa mfalme alimshitaki Tian Bao kwa baba yake, mwanzoni mfalme alipouliza alifikiri ni ugomvi wa kawaida tu kati ya mume na mke waliooana, alipuuza. Mhuni Chang Ming alikuwa siku zote alikuwa na chuki Tian Bao, alimshawishi mfalme amwue kutokana na ugomvi wao, mfalme alitaka kumwua Li Ying. Mama wa Tian Bao alimhurumia sana binti yake halisi, alimweleza ukweli wa mambo kwamba Li Ying ni binti Xu Dong, mfalme alighadhibika vibaya, alitaka kuinua familia ya Xu Dong na kumwua Tian Bao, aliyesimamia uuaji huo alikuwa Chang Ming.

Katika mahali pa kuulia, Li Ying na Tian Bao waliahidiana kuwa Tian Bao akiuawa Li Ying pia atajinyonga nyumbani. Lakini dakika kabla ya uuaji kutekelezwa, binti wa mfalme alikuja haraka na amri ya mfalme, kwamba Tian Bao amesamehewa adhabu ya kifo na aendelee kuwa mume wa binti yake. Lakini ngoma ilipigwa kuashiria uuaji ufanywe, Li Ying aliposikia vishindo vya ngoma alijinyonga. Tian Bao alimchukua Li Ying mikononi akipiga hatua pole pole huku akitokwa na machozi.

Fadhili ya Punda na Wema wa Kisura

Mganga aliyestaafu wa mfalme Zhou Hongde alikuwa na johari moja ambayo inaweza kugundua na kutibu magunjwa. Siku moja mafuriko yalipotokea mganga huyo alimwokoa kijana mmoja aitwaye Liao Zhongping na kumchukua kuwa ni mwana wake wa kulea. Wakati huo alipashwa habari kuwa mama mfalme anaumwa na dawa zote hazikumsaidia. Basi mganga mstaafu Zhou Hongde aliwaagiza mtoto wake halisi Yao Nian na mtoto wake wa kulea Liao Zhongping waende pamoja kwa mama mfalme wakiwa na johari yake. Ili kupata johari, njiani Liao Zhongping alimsukuma gengeni Yao Nian, na alienda kumganga mama mfalme kwa johari aliyoinyakua. Mama mfalme akapona, Liao Zhongping alirudi na sifa tele na mavazi ya fahari, aliteuliwa kuwa mtemi mkubwa, na alitangaza kuwa Yao Nian alianguka na kufa gengeni walipokuwa njiani, na alichoma moto nyumba ya baba yake mlezi Zhou Hongde na kumnyang'anya mtoto wa kike wa kulea Wan Qing kuwa mke wake, na huyo Wan Qing alijitupa mtoni kujiua.

Mganga mstaafu Zhou Hongde alikuwa mgonjwa kutokana na msiba na hasira, na alidaiwa madeni mengi kutokana na ugonjwa wake. Mke wa Zhou Zhaonian, Shu Xian, alilazimika kuolewa na jemadari mmoja aliyeitwa Xiong Yemeng kuwa mke wa pili ili aweze kuwaokoa wanafamilia wazee na watoto. Katika siku ya ndoa, jemadari Xiong Yemeng alipata amri ya kwenda kupambana na maadui mpakani, akamwagiza Shu Xian amlee mtoto wake mdogo Xiong He-en. Baada ya miaka minane, mtoto wake halisi Zhou Xiaoping na mtoto wa jemadari Xiong He-en walikuwa watu wazima na wote walikuwa maofisa. Na Zhou Zhaonian aliyesukumwa gengeni aliokolewa na amekuwa jemadari. Katika ushirikiano wa mapambano majemadari hao wawili waliweka urafiki mkubwa. Katika karamu ya kusherehekea ushindi Zhou Zhaonian alikutana na mkewe Shu Xian. Majemadari wawili hao waligombania mke. Baada ya kuelezana mambo yaliyopita, ukweli ukawa umedhihirika. Mwishowe Liao Zhongpia aliadhibiwa kisheria, na jemadari Xiong Yemeng alimwoa msichana Wan Qing aliyeokolewa kutoka mtoni. Jamaa wa familia ya Zhou wakajiunga pamoja.

Hawara Yang Guifei Alewa

Siku moja mfalme Xuanzong wa Enzi ya Tang, aliweka miadi na hawara yake Yang Guifei, kwamba wataburudika na maua na kunywa mvinyo katika kibanda cha Baihua. Katika siku ya miadi Yang Guifei alifika mapema kwenye kibanda cha Baihua na kuandaa tayari vyakula na mvinyo kwa furaha, lakini alimsubiri na kusubiri mfalme hakufika. Ghafla alikuja mtu kumwaarifu kuwa mfalme amekwenda kwa hawara wake mwingine Jiangfei, na hawezi kwenda kwake. Yang Guifei alisononeka sana baada ya kusikia habari hiyo. Yang Guifei ni mwanamke mwenye wivu na kujishaua. Alikunywa glasi tatu za mwinyo mfululizo akaanza kujirahisisha na kuwashawishi kijinsia matowashi wawili wa mfalme mpaka achoke sana na kurudi kwenye kasri.


1 2 3 4