Katika miaka mingi iliyopita, wachina walifuata desturi za kubana matumizi katika maisha yao, watu wenye desturi hizo walisifiwa kuwa ni watu waliofuata maadili, na watu waliotumia pesa ovyo walichukuliwa kuwa ni watu walioweza kuleta madhara kwa familia, hivyo watu wengi walibana matumizi katika maisha, na kila mara waliweka akiba benkini. Lakini hivi sasa China imeingia katika zama za matumizi, watu wengi wamebadilisha mtizamno wao kuhusu matumizi, na serikali pia inawahimiza watu waongeze matumizi ili kusaidia ongezeko la uchumi. Kila ifikapo sikukuu au siku za mapumziko, maduka ya mijini huandaa shughuli za kuhimiza ununuzi, watu wengi wanapenda kwenda madukani kununua nguo na vitu mbalimbali vya matumizi ya lazima, kununua vyombo vya umeme vya nyumbani, magari, au nyumba, ama kujiunga na ujumbe wa shirika la utalii kwenda nchi za nje kutalii, na vijana wengi wanapenda zaidi kutumia pesa zao kwa maisha yenye raha zaidi. Lakini kitendo cha kutumia pesa zaidi kuliko mapato yao kila mwezi hakikubaliwi na watu wengi.